1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mwisho wa juma Ujerumani jaribio kwa Scholz?

9 Oktoba 2023

Muungano wa vyama vitatu vinavyounda serikali ya Ujerumani inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz wa chama cha SPD, umepata hasara kubwa katika uchaguzi wa majimbo mawili siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/4XIeS
Vipeperushi vya  wagombea wa kisiasa wa vyama mbalimbali
Vipeperushi vya wagombea wa kisiasa wa vyama mbalimbaliPicha: Florian Gaul/greatif/IMAGO

Kulingana na makadirio ya kura, vyama vyote vitatu vinavyounda serikali ya muungano: SPD cha Kansela Scholz, chama cha Kijani kinachowakilisha walinzi wa mazingira na FDP kinachowakilisha maslahi ya wafanyabiashara, vimeshindwa katika jimbo kubwa kabisa nchini Ujerumani na Hesse magharibi.

Matokeo ya awali yanaashiria kwamba kama ilivyotarajiwa, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, AfD, kimezidi kujiimarisha.

Soma pia:Vyama ndugu vya kihafidhina, Christian Social Union CSU, na Christian Democratic Union nchini Ujerumani vyashinda katika chaguzi za kijimbo

Chaguzi hizo zilionekana kama kipimo muhimu cha muitikio wa watu, huku ajenda kuu ikiwa kuongezeka kwa uhamiaji pamoja na matatizo ya kiuchumi.

Wapiga kura katika majimbo mawili tajiri, Bavaria na Hesse, wamevipa ushindi vyama ndugu vya kihafidhina, Christian Social Union CSU, na Christian Democratic Union. 

Matokeo ya uchaguzi yazua gumzo

Matokeo duni katika muungano unaosuasua wa Scholz, yameibua gumzo miongoni mwa viongozi wakuu, wakikubaliana kwamba mbinu mpya inahitajika.

Kiongozi mwenza wa SPD, Lars Klingbeil, aliliambia shirika la utangazaji la Ujerumani ARD kwamba uchaguzi huo ulikuwa kile alichokitaja kama "ishara kwa muungano wao kwamba kasi tofauti inahitajika linapokuja suala la kutatua matatizo ya wananchi."

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser ambaye hakufanikiwa kuwa Waziri Mkuu wa jimbo la Hesse baada ya kushindwa matokeo haya ya uchaguzi yanakatisha tamaa sana.

Waziri wa Mambo ya ndani Ujerumani Nancy Faeser
Waziri wa Mambo ya ndani Ujerumani Nancy FaeserPicha: Boris Roessler/dpa/picture alliance

Aliongeza kwamba walikuwa na tumani katika kampeni kwamba wangeliweza kuongoza serikali ya majimbo ya baadaye.

"Kwa bahati mbaya, hatukuweza kufanikiwa, malengo yetu kama vile huduma ya kulelea watoto bila malipo kwa wote hata chini ya umri wa miaka mitatu, ili iwe Hesse ya kijamii zaidi yenye malazi ya bei nafuu, yenye huduma nzuri ya afya kwa kila mtu na pia jinsi gani tutahakikisha ajira katika siku zijazo. Na ndio maana ni matokeo ya kukatisha tamaa sana.”

Kinyume chake, kulikuwa na sababu ya kusherehekea katika chama cha AfD inayopinga uhamiaji.

Soma pia:AfD kuamua wagombea wake katika bunge la Ulaya

Kiongozi mwenza, Alice Weidel, alitangaza kuwa chama hicho kilikuwa "katika njia sahihi", akiutaja uchaguzi wa jana Jumapili kama "kura ya mabadiliko na somo kwa muungano wa SPD".

Waziri kiongozi wa jimbo la Bavaria, Markus Soeder kutoka chama cha CSU, amesema matokeo ya uchaguzi wa majimbo hayo mawili ni ishara kwamba raia wa Ujerumani wanataka sera mpya na imara zaidi kuhusu wahamiaji.

Chama cha AfD kilichoshika nafasi ya pilibaada ya wahafidhina katika chaguzi hizi, kinapinga vikali wahamiaji.

Uchaguzi huo unajiri baada ya miaka miwili mibaya kwa serikali ya Scholz, ambayo imelazimika kukabiliana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na mzozo wa nishati uliofuata, ambao uliitumbukiza Ujerumani katika mdororo wa kiuchumi.

Mbali na haya muungano wa kansela Scholz umegubikwa na mgogoro mkali katika masuala mbalimbali kuanzia sheria za mabadiliko ya tabianchi hadi kubana matumizi.
 

Wapiga kura wa mara ya kwanza hawafurahii matokeo ya uchaguzi