Mifumo ya kompyuta Ujerumani yadukuliwa
1 Machi 2018Kamati ya masuala ya dijitali ya bunge la Ujerumani imeitisha mkutano wa dharura baadaye leo kupitia taarifa juu ya udukuzi huu na kutoa rasmi madai ya kupatiwa undani wa uchunguzi juu ya mashambulizi hayo, ambayo ndiyo kwanza yalifahamika jana, Jumatano.
"Ikiwa serikali ilifahamu kuhusiana na udukuzi huu tangu mwezi Disemba, ukweli kwamba wabunge wenye dhamana ya kusimamia masuala ya dijitali walilazimika kuyajuwa kupitia vyombo vya habari ni kashfa kubwa," alisema Anke Domscheit-Berg, mjumbe wa kamati hiyo kutokea chama cha mrengo wa kushoto, Die Linke.
Shirika la habari la Ujerumani, dpa, lilivinukuu vyanzo vya usalama ambavyo havikutajwa majina vikisema kwamba kundi la APT28 la Urusi lilidukuwa mifumo ya mawasiliano ya wizara za mambo ya nje na ndani za Ujerumani na kufanikiwa kuiba data.
Shirika hilo linasema kuwa mashambulizi hayo yaligunduliwa mwezi Disemba mwaka jana na inawezekana yalikuwa yakiendelea kwa mwaka mzima.
Serikali yakiri udukuzi
Kufuatia ripoti hiyo, wizara ya mambo ya ndani ilithibitisha kudukuliwa kwa kompyuta za serikali kuu ya shirikisho, ikisema kuwa mashambulizi hayo yalifanyika kwenye masuala yasiyohusiana na siri za serikali na kwamba yalidhibitiwa.
Hata hivyo, msemaji wa wizara hiyo hakuweza kutoa undani zaidi wa suala hili, akisema limo kwenye uchunguzi na kwamba hatua za kiusalama zinaendelea kuchukuliwa.
Lakini kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ujerumani, udukuzi uliachiwa kuendelea hadi jana (Jumatano, 28 Februari) ili wachunguzi wakusanye taarifa kuhusiana na upana, malengo na watendani wenyewe.
"Ikithibitika kuwa ni kweli, hivi vitakuwa ni aina ya vita dhidi ya Ujerumani," alisema mkuu wa kamati ya masuala ya dijitali ya bunge la Ujerumani, Dieter Janacek, kutoka chama cha walinzi wa mazigira, Die Grüne, kwa mujibu wa gazeti la Berliner Zeitung.
Janacek aliyataja mashambulizi hayo kubwa ni mabaya kabisa, na ametoa wito kwa serikali kuzifikisha taarifa zote ilizonazo bungeni.
Alipoulizwa endapo mashambulizi hayo yalifanywa na kundi linaloungwa mkono na Urusi, mbunge kutokea muungano wa CDU/CSU wa Kansela Angela Merkel, aliutetea mkakati wa serikali kuzuia taarifa. Stephan Mayer kutoka chama cha CSU alisema "uchunguzi kamili na wa kina" ulikuwa unahitajika "lakini sio wa kuwekwa hadharani." Mbunge huyo aliongeza kuwa "kuwadhania vibaya wengine hakuwezi kuusaidia uchunguzi huo".
Kundi la APT28 au wakati mwengine huitwa Fancy Bear, ambalo linahusishwa na idara ya ujasusi kwenye jeshi la Urusi, limewahi kutajwa kuhusika na mashambulizi ya mtandaoni dhidi ya Bunge la Ujerumani mwaka 2015 na pia ofisi za Jumuiya ya Kujihami ya NATO na serikali za mashariki mwa Ulaya.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Saumu Yusuf