Miguna Miguna azuiliwa tena kurudi kwao Kenya
16 Novemba 2021Miguna alitarajiwa kuwasili nchini Kenya mapema asubuhi ya Jumanne (16 Novemba 2021), licha ya mwenyewe kukiri kufahamu kuhusu hatua ya kuzuiliwa kwake kurejea Kenya katika uwanja wa ndege wa Berlin nchini Ujerumani.
Ndege iliyokuwa imbebe ilistahili kutoka Canada kupitia Ujerumani na Ufaransa kisha itue katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mwendo wa saa 3:00 asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki.
Kuzuiwa kwa Miguna kunakuja hata baada ya Mahakama Kuu kukataa kuondoa kibali cha kutosafiri kwa wakili huyo siku Ijumaa kilichotolewa na serikali ya Kenya dhidi yake.
Kupitia wakili wake, John Khaminwa, Miguna amesama kuwa vibali vilivyotolewa viliyazuia mashirika ya ndege ya Lufthansa na Air France kutomsafirisha kuingia nchini Kenya tarehe 16 mwezi Novemba ama siku nyingine yoyote.
Ugomvi wa Miguna na serikali?
Akihojiwa na shirika moja la habari nchini Kenya, Miguna alidai kuwa sababu ya kuzuiliwa kuingia kwake inatokana na ukweli kuwa ana ufahamu kuwa Rais Uhuru Kenyatta aliiba kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, ambapo yeye Miguna alimuapisha kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwa rais baadaye, hatua ambayo ilionekana kukiuka sheria za nchi.
"Uwoga unaweza ukafanya ukachukua maamuzi yasiyo na hekima, hayana msingi, yaliyo na nia mbaya, na ndivyo anavyofanya Uhuru Kenyatta." Alisema mwanaharakati huyo.
Miguna, ambaye pia ni wakili mwenye uraia wa Kenya na wa Canada, alitimuliwa nchini Kenya tarehe 6 Februari 2018 na serikali kwa madai kuwa aliukana uraia wake wa Kenya.
Hata hivyo, aliwasilisha ombi mahakamani ambapo mahakama iliamua kuwa hatua ya serikali ya kumtimua ilikiuka sheria na katiba ya nchi.
Jaribio lake la kwanza kurejea nchini Kenya mwezi Machi 2018 lilikataliwa alipotua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, ambapo alirejeshwa kwa nguvu nchini Canada.
Kundi la vuguvugu likiongozwa na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, Nelson Havi, na aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, limefika mahakamani likitaka amri ya kumzuia Miguna kurejea nchini kuondolewa.
"Suala sio iwapo wanampenda Miguna ama la. Kesi ya Miguna inatisha, kwamba mahakama inaweza kufanya uamuzi unaokupendelea na hayazingatiwi, yaweza kufanyikia ama kunifanyikia," alisema Jaji Mstaafu Mutunga.
Mwezi Oktoba Mutunga alitangaza kuwa angekwenda mjini Toronto ambapo angeandamana na Miguna kwa safari ya kurejea nchini.
Imetayarishwa na Shisia Wasilwa, DW Nairobi