1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Gaza: Israel yaelekeza mashambulio Lebanon

Zainab Aziz Mhariri:Gakuba, Daniel
19 Mei 2021

Israeli imesema haitaweka muda wa kusitisha mzozo kati yake na Hamas. Wakati huo huo makombora yamerushwa kuelekea Israel nayo imejibu kwa kuishambulia Lebanon. 

https://p.dw.com/p/3tczI
Weltspiegel 19.05.2021 | Nahostkonflikt | Aschkelon Raketenabwehr Iron Dome
Picha: Amir Cohen/REUTERS

Maafisa wa matibabu wa Palestina wamesema watu 219 wameuawa hadi kufikia sasa katika muda wa siku 10 ambapo sehemu za raia na miundominu mingine imeshambuliwa kwenye Ukanda wa Gaza, yote hayo yakiwa yanaongeza hali mbaya ya kibinadamu iliyokuwepo katika eneo hilo.  Taarifa za hivi punde zinafahamisha kwamba Israel imeshambulia upande wa Lebanon kulipiza mashambuliom ya roketi.

Kulingana na taarifa ya msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, watu zaidi ya elfu 58 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mashambulio ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.

Katika mashambulio yaliyochukua dakika 25 usiku wa kuamkia leo wanajeshi wa Israeli walipiga maeneo ya wapiganaji wa Hamas na mahandaki yapatayo 40 kusini mwa Ukanda wa gaza.

Wokoaji wa Palestina wakikagua uharibifu nje ya jengo la makazi lililoharibiwa kutokana na mashambulizi ya anga ya Israeli
Wokoaji wa Palestina wakikagua uharibifu nje ya jengo la makazi lililoharibiwa kutokana na mashambulizi ya anga ya IsraeliPicha: AFP via Getty Images

Mamlaka ya Israeli imesema idadi ya watu waliokufa nchini humo ni 12, kutokana na mashambulizi ya roketi kutokea kwenye Ukanda wa Gaza ambayo yamesababisha hofu na kuwafanya watu kukimbilia kwenye sehemu za kujikinga.

Jitihada za kidiplomasia za Kikanda na Marekani juu ya kusimamisha mapigano hadi sasa hazijafua dafu.  Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipozungumza na mabalozi wan chi mbalimbali hakutamka juu ya kusimamisha mapigano ila alisema nchi yake inapambana sasa ili kuzuia mzozo wa siku zijazo kati ya Israel na kundi la wapiganaji wa Hamas.

Chanzo:/RTRE