1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko ya mabomu yaua 115 Pakistan

MjahidA11 Januari 2013

Zaidi ya watu 115 wameuwawa katika mashambulizi yanayohusishwa na tafauti za kimadhehebu nchini Pakistan, na yanayotajwa kuifanya jana kuwa moja kati ya siku za umwagikaji mkubwa wa damu nchini humo

https://p.dw.com/p/17Ho2
Hasara ya mashambulizi Pakistan
Hasara ya mashambulizi PakistanPicha: Reuters

Takriban watu 115 waliuwawa hapo jana na wengine 121 wakajeruhiwa baada ya washambuliaji wawili wa kujitoa muhanga waliolenga mahali palipojaa watu kujilipua kusini magharibi mwa mji wa Quetta, mji ambao unakaliwa na watu wa madhehebu ya Shia.

Kundi lililo la itikadi kali la Kiislamu la Sunni la Lashkar-e-Jhangvi lilikiri kufanya mashambulizi hayo. Kundi hilo la kisunni lenye itikadi kali linawalenga waumini wa madhehebu ya Shia, ambao wanachangia asilimia 20 ya raia wa Pakistan.

Baadhi ya polisi Afghanistan
Baadhi ya polisi AfghanistanPicha: Reuters

Mashambulizi hayo yanadhihirisha ukubwa wa kitisho kinacholikabili jeshi la Pakistan kutoka kwa makundi ya Kisunni yenye msimamo mkali, kundi la Taliban kaskazini magharibi na kundi lingine la uasi lisilojulikana sana la Baluchi, kusini-magharibi mwa Pakistan.

Kulingana na wakaazi wa mji wa Quetta bomu la kwanza liliruka kwenye klabu moja na kusababisha mauaji ya watu 100 kisha baada ya dakika 10 bomu lingine lililotegwa ndani ya gari likaripuka na kuuwa maafisa watano wa polisi.

"Niliskia sauti ya mripuko mkubwa nyuma yangu, nilidondoka kutoka kwenye pikipiki na nilivyoinuka niliona moshi mkubwa ambao ulionekana kama wingu jeusi angani." Alisema Abdul Basit mkaazi wa mji wa Quetta.

Mauaji na mashamabulizi ya mabomu dhidi ya jamii za Washia ni ya kawaida nchini Pakistan, na makundi ya haki za binaadamu yanasema mamia ya Washia waliuawa mwaka uliyopita. Makundi yenye silaha jimboni Baluchistan yanawaua mara kwa mara abiria wa Kishia kwenye mabasi wakiwa safarini kuelekea nchi jirani ya Iran.

Lawama kwa serikali ya Pakistan

Wakaazi wakiomboleza baada ya mashambulizi
Wakaazi wakiomboleza baada ya mashambuliziPicha: AP

Hata hivyo baadhi ya wakaazi wa Pakistan wanatoa lawama zao kwa vikosi vya serikali jimboni mwao, kama sababu ya mashambulizi haya ya mara kwa mara. "Hakuna serikali hapa, mashambulizi ya bomu ya kila siku yamekuwa ya kawaida na serikali haifanyi chochote. Hatutaki wanajeshi mjini humu, tunashambuliwa kwa sababu yao" Alisema Abdul Raheem Kakar
Lakini wasi wasi wa kiitikadi siyo chanzo pekee cha vurugu. Jimbo la Baluchistan ni eneo la mgogoro wa karibu muongo mzima dhidi ya serikali ya Pakistan.

Wanachama wa kundi la Taliban
Wanachama wa kundi la TalibanPicha: dapd

Waasi wa United Baluch Army walidai kuhusika na mashambulizi yaliyouwa watu 11 na kujeruhi zaidi ya 40 katika soko la Quetta mapena jana. Kundi hilo linataka uhuru zaidi wa kisiasa, na mgao mkubwa wa faida inayotokana na rasilimali za mafuta za gesi vinavyopatikana jimboni mwao.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef