Misaada ya kimataifa imeanza kumiminika Myanmar
12 Mei 2008Sasa,ndio misaada ya kimataifa imeanza kumiminika nchini Myanmar na hivyo kuleta matumaini mapya kwa kiasi ya watu milioni moja na nusu wanaohitaji misaada hiyo kwa dharura.Juu ya hivyo,viongozi wa kijeshi nchini Myanmar wamesema,wataalamu wa kigeni wenye ujuzi wa kusismamia misaada wakati wa maafa makubwa kama hayo,hawatoruhusiwa kuongoza kazi za ugavi.Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Myanmar,Soe Tha amenukuliwa akisema kuwa kazi ya kugawa misaada hiyo inaweza kutekelezwa na mashirika ya kienyeji.Kwa mujibu wa waziri huyo, helikopta hazikuweza kutua sehemu hizo kwa sababu ya mafuriko na vyakula vilidondoshwa kutoka juu.
Lakini mashirika ya kigeni yanayotoa misaada,yanashikilia kuwa serikali ya Myanmar haina uwezo wa kuongoza huduma za ugavi wa misaada hiyo,hasa katika eneo la mdomo wa mto kusini mwa nchi,lililoteketezwa na kimbunga cha Mei 3.Tatizo jingine ni kuwa sasa kuna hatari nyingine,kwani magonjwa yameanza kuwa kitisho kikubwa kwa wale walionusurika na wanaoishi katika hali za kusikitisha sana.Katika sehemu hizo,watu hawana chakula cha kutosha wala maji safi.Maiti za binadamu na mifugo bado zinaelea majini na kusababisha hatari kubwa ya magonjwa.
Samson Jeyakumar wa "World Vision"-shirika mojawapo la misaada amesema:
"Tumeshapata habari kuwa tayari kunaripotiwa kesi za kuharisha.Sasa ni suala la wakati tu kwa ugonjwa wa kipindupindu kutokea sehemu hizo. Ugonjwa huo unaweza kutokea wakati wo wote."
Watu wengi katika eneo hilo la kusini wanasikitika kuwa hawajapokea msaada wo wote wa dharura kutoka serikalini.Viongozi wa kijeshi wanaotawala kwa mabavu nchini Myanmar tangu miaka 46,walikataa kupokea misaada kutoka nje licha ya shinikizo kubwa la jumuiya ya kimataifa.Sasa ndio imeruhusu misaada hiyo kupelekwa hadi mji mkuu Rangoon kwa sharti kuwa serikali ndio itakayosimamia ugavi. Wataalamu wa kimataifa wananyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo.Meja Tom Keating wa jeshi la wanamaji la Marekani alipozungumza leo hii kabla ya ndege ya Marekani kuelekea Yangon na mizigo ya mablanketi,vyandarua na maji alisema,ni jambo linalovunja moyo kuona mzozo wa kibinadamu ukiendelea na hakuna ruhusa ya kusaidia.
Ingawa hivi sasa,misaada ya kimataifa imeanza kumiminika kwenye uwanja wa ndege wa Yangon, mashirika ya kimataifa yanayotoa misaada,yanasisitiza kuwa misaada zaidi inahitajiwa.Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kati ya watu milioni 1.2 hadi milioni 1.9 wanapigania maisha yao.Serikali ya Myanmar inasema,watu 28,000 wameuawa katika kimbunga Nargis,lakini mashirika ya kimataifa yanahofu kuwa idadi ya watu waliouawa huenda ikapindukia 100,000.Vile vile kama watu 220,000 hawajulikani walipo.