1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misiri na Nigeria nani atatamba leo Benguela ?

12 Januari 2010

Msumbiji na Benin ni changamoto nyengine leo.

https://p.dw.com/p/LRer
CAF yaitoa Togo mashindanoni Angola.Picha: AP

KOMBE LA AFRIKA LZUSHA MSANGAO:

Michuano ya Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola, yanaendelea jioni ya leo huko Benguela, kwa mapambano 2: Mabingwa Misri wanaanza kampeni yao ya kutwaa Kombe hili kwa mara ya 3 mfululizo, wakati mahasimu wao, Nigeria,wanajiwinda kuwavua taji na mapema.Baadae itakua zamu ya Msumbiji na Benin, kila moja kuandika historia kwa kujipatia ushindi wa kwanza katika kombe la Afrika.

Mapambano 2 ya jana yalimalizika kwa msangao-Malawi ikiinyoa Algeria bila ya maji kwa mabao 3:0 wakati Burkina Faso, ilichachamaa isikanyagwe na Tembo wa Ivory Coast. Usalama katika kombe lijalo la dunia Juni hii ijayo nchini Afrika kusini, ni mada pia inayogonga vichwa vya habari baada ya msiba ulioikumba Togo huko Kabinda.

MABINGWA MISRI:

Mabingwa (mafiraouni) Misri ,wana kibarua kigumu leo kuuvunja ubishi wa super Eagles-Nigeria- huko Benguela na kurejesha heshima yao iliovunjwa na Algeria walipoipiga kumbo huko Khartoum, Novemba mwaka jana, nje ya Kombe la dunia. Misri halkadhalika inapaswa kuhimili pigo la kuumia kwa mastadi wake wengi. Hata hivyo, wao ndio mabingwa mara 6 wa Afrika na ndio wanaopigiwa upatu kuondoka na Kombe ikiwa Nigeria leo haitawatia munda.

Timu hizi mbili zikiaga uwanja, itakua zamu ya chipukizi 2 wa kombe hili: Msumbiji na Benin, huku kila moja ikitaka kuiigiza malawi jana alao kuondoka na ushindi mmoja. Benin ilishindwa mechi zake zote 6 katika vikombe viwili vilivyopita ilipocheza. Rekodi ya Msumbiji : ni kutoka sare mara 1 na kushindwa mara 8 iliposhiriki katika vikombe 3 vilivyopita.

Mshangao ulizuka jana katika Kombe hili la Afrika pale Malawi, timu chipukizi, ilipotamba mbele ya Waalgeria, timu iliowapiga kumbo mabingwa wa Afrika nje ya Kombe lijalo la dunia. Kwa mabao 3:0,Algeria,ni hamkani haijui kilipita nini uwanjani. Hata Tembo wa Corte d'Iviore pamoja na nahodha wao, Didier Drogba, hawakuwa na ufunguo jana kuvunja tumbuu ya langola Burkina Faso.Mwishoe, waliondoka suluhu 0:0.

HATIMA YA GHANA:

Baada ya kutolewa mashindanoni kwa Togo,kufuatia kurudi kwake nyumbani kuomboleza msiba na kutotimiza miadi yake ya kucheza na Ghana jana usiku huko Cabinda, Ghana inabidi kupumzika hadi changamoto yake ya Ijumaa hii na Ivory Coast. Huo kwa Ghana,utakuwa kwake na hata Ivory Coast, mpambano wa kufa-kupona,kwani katika kundi hili la timu 3,kila moja haimudu kushindwa.

USALAMA:

Usalama katika Kombe hili la Afrika na lijalo la dunia nchi jirani Afrika kusini, ungali ni mada kuu inayozungumzwa na sio tu Afrika: Mkuu wa Kamati ya Maandalio ya Kombe lijalo la Dunia huko Afrika Kusini, Danny Jordaan, amesema leo kwamba, Afrika Kusini ihukumiwe kwa rekodi yake na sio visa vilivyozuka masaa 4 ya safari ya ndege. Jordaan amesema kuwa, Afrika Kusini, imeshaandaa zaidi ya mashindano makuu 100 tangu kumalizika ubaguzi na mtengano-aparthied-1994 tena bila kuzuka machafuko viwanjani.

Angola kwenyewe, kikundi cha pili cha waasi kimejitwika jukumu la kulifyatulia risasi basi la timu ya Togo.FLEC-FAC kundi kubwa zaidi la ukombozi wa Cabinda,leo limechukua dhamana ya shambulio lile.Angola imesema mapambano yote yaliosalia, yataendelea kuchezwa Cabinda.

Mwandishi:Ramadhan Ali /AFPE/APE

Uhariri: Miraji Othman