1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiEthiopia

Misri, Ethiopia zaanza tena mazungumzo ujenzi wa bwawa

28 Agosti 2023

Misri imetangaza kwamba mazungumzo yameanza tena kuhusu bwawa kubwa la Ethiopia baada ya viongozi wa nchi hizo mbili kukubaliana mwezi uliopita kufikia makubaliano kufuatia miaka mingi ya mvutano kati ya nchi hizo mbili

https://p.dw.com/p/4VevT
Bwawa la Grand Renaissance nchini Ethiopia, kiwanda kikubwa cha kuzalisha umeme unaotokana na maji kwenye Mto Nile linalopakana na Sudan na Misri, wakati bwawa hilo lilipoanza kuzalisha umeme huko Benishangul-Gumuz, Ethiopia mnamo Februari 19, 2022.
Bwawa la Grand Renaissance nchini EthiopiaPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Viongozi hao wawili walikutana  pembezoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika kutoka mataifa jirani na Sudan inayokumbwa na vita, wanaotafuta kumaliza mzozo ambao umedumu nchini humo kwa zaidi ya miezi minne.

Misri yataka makubaliano ya kisheria

Wizara ya Rasilimali za Maji na umwagiliaji ya Misri imetangaza kuwa duru mpya ya mazungumzo kuhusu bwawa la Grand Renaissance yalianza Jumapili (27.08.2023) asubuhi mjini Cairo na  kushirikisha wajumbe wa Misri, Sudan na Ethiopia. Waziri wa wizara hiyo Hani Sewilam, amesema kwamba Misri inataka makubaliano ya kisheria kuhusu jinsi bwawa hilo kubwa litakavyoendeshwa na kujazwa.

Soma pia:Bwawa kubwa la utata la Ethiopia

Sewilam amesema kuna suluhu nyingi za kiufundi na kisheria katika mzozo huo lakini hakutoa ufafanuzi zaidi. Sewilam amesema mazungumo ya sasa yanalenga kufikia makubaliano ambayo yanazingatia maslahi ya mataifa hayo matatu, akihimiza kusitishwa kwa hatua za pande moja.

Misri yautegemea mto Nile kwa kiasi kikubwa

Bwawa hilo kubwa la Ethiopian lenye thamani ya dola bilioni 4.2 limekuwa suala kuu la mzozo wa kikanda tangu Ethiopia ilipoanzisha msingi wa mradi huo mwaka 2011, huku Misri ikihofia kuchukuliwa kwa sehemu yake katika mto Nile. Misri inahofia athari mbaya ikiwa bwawa hilo litaendeshwa bila kuzingatiwa kwa mahitaji yake. Taifa hilo, imeliita bwawa hilo tishio lililopo. Misri, taifa la kiarabu lenye idadi kubwa zaidi ya watu, hutegemea mto Nile kwa kiasi kikubwa zaidi kusambaza maji kwa shughuli za kilimo na matumizi ya watu wake ambao ni zaidi ya milioni 100.

Soma pia: Mazungumzo kuhusu ujenzi wa bwawa la umeme la GERD yamekwama

Takriban asilimia 85 ya maji ya mto huo hutokea Ethiopia.

Mandhari ya kuvutia ya mto Nile mjini Aswan nchini Misri
Mto Nile nchini MisriPicha: Kokhanchikov/Zoonar/picture alliance

Bado kuna maswali yanayohitaji kujibiwa kuhusu bwawa la Grand Renaissance

Mvutano umeongezeka kati ya Misri na Ethiopia baada ya serikali ya Ethiopia kuanza kujaza hifadhi ya bwawa hilo kabla kufikia makubaliano. Bado kuna maswali muhimu kuhusu kiasi cha maji ambacho Ethiopia itatoa kuelekea kwa mto Nile ikiwa ukame wa  miaka mingi utatokea na jinsi mataifa hayo matatu yatakavyosuluhisha mizozo yoyote katika siku zijazo. Ethiopia imekataa suluhisho la makubaliano ya kisheria katika hatua ya mwisho ya mradi huo.

Soma pia: Ethiopia, Misri, Sudan zakubali kuahirishwa ujazaji wa bwawa la Nile

Ethiopia inasema bwawa hilo ni muhimu, na kuongeza kuwa watu wake wengi hawana umeme.

Ethiopia yatakiwa kubadilishana data kuhusu bwawa la Grand Renaissance

Sudan inataka Ethiopia kuratibu na kubadilishana data kuhusu operesheni za bwawa hilo lililoko umbali wa kilomita 10 tu kutoka mpaka wa Sudan ili kuepuka mafuriko na kulinda mabwawa yake ya kuzalisha umeme katika mto Blue Nile.

Tangu mwaka 2011 hadi sasa, mazungumzo ya muda mrefu kuhusu kujazwa na  kuendeshwa kwa  bwawa hilo yameshindwa kuleta makubaliano kati ya Ethiopia na majirani zake Misri na Sudan.