Misri katika kingo
25 Julai 2013Polisi imesema inapanga kupeleka maelfu ya wanajeshi kulinda mikutano hiyo iliyoitishwa siku ya Ijumaa, ambayo inazua wasiwasi wa umuagaji zaidi wa damu kati ya wafuasi wa vyama vya Kiislamu wanaodai kurejeshwa madarakani kwa rais Mohammad Mursi, na wapinzani wao ambao sasa wanahusisha jeshi la nchi hiyo. Kiongozi anayesakwa wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu la rais Mursi, Mohamed Badei, ametoa wito kwa Wamisri kusima imara lakini kwa amani, kwa ajili ya uhuru na sheria, na dhidi ya mapinduzi ya umuagaji damu.
Marekani yasitisha mauzo ya ndege za kivita
Marekani ilisema siku ya Jumatano kuwa ina wasiwasi mkubwa na wito wa maandamano uliyotolewa na mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Sisi, kuhalalisha ukandamizaji dhidi ya kile alichokiita "ugaidi na vurugu." Marekani ambayo ina uhusiano wa karibu na jeshi la Misri, ilitangaza kusitisha mpango wa kuiuzia nchi hiyo ndege za kivita aina ya F-16. Udugu wa Kiislamu na vyama vingine washirika wamelaani wito uliotolewa na Al-Sisi na kuuita tangazao la vita vya wenyewe kwa wenyewe, huku wakisistiza kuendelea na maandamano yao siku ya Ijumaa.
Magazeti ya Misri, ambayo yana uadui na Udugu wa kiislamu yalichapicha habari ya wito wa Al-Sisi katika kurasa zake za mbele. Gazeti linalomilikiwa na serikali la Al-Akhbar lilichapisha habari yenye kichwa kilichokolezwa kwa rangi nyekundu kikisomeka kuwa: Ujumbe wa Sisi umefika. Na watu wakaitika: Tunakupa mamlaka." Gazeti huru la Al-Masry al-Yaum liliandika kichwa kisemacho: "Sis anatoa wito. Na watu wanaitika."
Fatwa yatolewa dhidi ya wito wa Al-Sisi
Nchini Qatar, shirika la Kiislamu linaloongozwa na mhubiri mwenye ushawishi mkubwa, ambae ni mzaliwa wa Misri Yusuf al-Qaradawi, lilitoa fatwa dhidi ya kutii wito wa Sisi, na kusema unaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Matakwa ya Jenerali huyo yasiyo ya kawaida, ambae jeshi linasisitiza kuwa yeye ni waziri tu wa ulinzi na naibu waziri mkuu katika serikali iliyowekwa madarakani na jeshi, yamekuja baada ya kutolewa miito ya ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa vyama wa vya Kiislamu, ambao wamekuwa wakiandamana tangu mapinduzi ya Julai 3.
Muda mfupi baada ya al-Sisi kutoa tamko la kuitisha maandamano, msemaji wa rais aliyewekwa na jeshi, Adly Mansour, alisema kuwa Misri imeanza "vita dhidi ya ugaidi." Zaidi ya watu 170 wameuawa katika machafuko ya kisiasa nchini Misri tangu mwishoni mw amwezi Juni, wengi wao wakiuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa Mursi na wapinzani. Kiongozi mwandamizi wa Udugu wa Kiislamu Essam al-Erian, alisema wafuasi wa Mursi hawatababaishwa na wito wa mkuu wa jeshi, wa kufanyika kwa maandamano makubwa.
Familia ya Mursi kumshtaki Al-Sisi
Kuzuiwa kwa Mursi na kukamatwa kwa viongozi waandamizi wa Udugu wa Kiislamu kumeimarisha msimamo wa wafuasi wake. Familia yake ilisema itamshtaki Sisi na itachukua hatua za kisheria nje ya Misri. Marekani imeungana na mataifa mengine kutaka kuachiwa kwa Mursi, ingawa imesita kukuita kuangushwa kwake kuwa ni mapinduzi, hatua ambayo inaweza kulaazimu kusimamisha msaada wa Marekani.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, ape
Mhariri: Mohamed Abudl-Rahman