1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri wahitimisha kampeni

Admin.WagnerD21 Mei 2012

Kampeni za uchaguzi wa rais nchini Misri zimemalizika huku matokeo ya kura za Wamisri walioko nje yakionyesha mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislam Mohammed Mursi akiongoza kwa kupata kura zaidi ya laki moja.

https://p.dw.com/p/14zWA
Kampeni za Muhammad Mursi.
Kampeni za Muhammad Mursi.Picha: AP

Wamisri walioko nje ya taifa hilo walipiga kura ya mapema ikilinganishwa na wenzao walioko nyumbani ambao wanatarajia kuhudhuria katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumatano na Alhamis na hivi sasa balozi za Misri zilizoko nje zimeanza kutoa matokeo ya uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa matokeo yaliotangazwa na balozi 33, Muhammed Mursi anaongoza kwa kura 106,252 akifuatiwa na Abdul Moneim Abul Futouh mwenye kura 77,499 wakati Mgombea mwingine anayepewa nafasi kubwa, Amr Mousa akishika nafasi ya nne nyuma ya Hamdeen Sabbahi aliyepata kura 44,727.

Mursi azoa kura nyingi Saudia Arabia na Kuwait
Kura nyingi alizozipata mgombea huyo wa chama cha Udugu wa Kiislam zilitoka kwa Wamisri walioko nchini Saudi Arabia na nyingine kutoka nchini Kuwait, mataifa mawili yaliyo na Wamisri wengi. Ingawa matokeo haya siyo rasmi, lakini yamefuatiliwa kwa karibu sana na wapiga kura walioko nchini Misri kwenyewe ambako kura za maoni zimekuwa zikitoa majibu ya kukanganya na yasiyo aminika.

Barani Uropa, matokeo yalitofautiana ambapo Sabbahi, anayetaka kurejesha sera za mrengo wa Kushoto za rais wa zamani wa Misri Gamal Nasser alishinda nchini Ufaransa akifuatiwa na Waziri Mkuu wa zamani Ahmed Shafiq. Nchini Uingereza, Abdul Futouh alishinda kwa kura 1,300 akifuatiwa na Sabbahi wakati nchini Ugiriki Amr Mousa aliongoza kwa kura 362 akifuatiwa na Shafiq na Sabbahi.

Wamisri wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeni.
Wamisri wakiwa katika moja ya mikutano ya kampeniPicha: Reuters

Takribani watu milioni 50 wanatizamiwa kushiriki katika uchaguzi huu wa kwanza huku serikali ikihaha kuimarisha usalama katika taifa hili ambalo limeshuhudia uvunjivu wa amani tangu kuanza kwa mandamano yaliomngoa rais Hosni Mubarak zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Waziri wa mambo ya Ndani wa Misri Mohammed Ibrahim alisema vikosi vya usalama vitawekwa katika vituo vyote 351 ambako kura zitahesabiwa.

Pande zinazovutana katika uchaguzi huu
Vuta nikuvute katika uchaguzi huu ni kati ya wagombea wa kiislam na wale wasioegemea dini, wanamapinduzi na wanachama wa utawala uliopita, na kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, matokeo ya uchaguzi hayajulikani. Mgombea wa Udugu wa Kiislam Muhammed Mursi alionya siku ya Jumapili dhidi ya udanganyifu katika mkutano wake uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi.

Amr Mousa naye aliwambia waandishi wa habari kuwa kampeni zake zilikuwa zikizidi kuungwa mkono, siku moja baada ya Abul Futouh kufanya Mkutano wa mwisho Mjini Cairo na kuahidi kuwaunganisha Wamisri. matokeo ya kura za maoni yaliondeshwa na shirika la ushauri linalofadhiliwa na serikali yalionyesha kuwa Mursi alikuwa nyuma ya Abul Futouh, Muosa na Shafiq.

Baraza la utawala la kijeshi limeahidi kukabidhi mamlaka kwa rais atakayechaguliwa na kiongozi wa Baraza hilo, Field Marshal Hussein Tantawi ameahidi kuwa watasimamia ahadi yao.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\
Mhariri: Saum Yusuf