1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaapa kuchukua hatua kali kufuatia mauaji ya Sinai

Josephat Nyiro Charo6 Agosti 2012

Misri imetangaza inakifunga kivuko cha mpaka wake na Ukanda wa Gaza cha Rafah kwa muda usiojulikana baada ya maafisa wake 16 wa polisi kuuwawa kwenye shambulio dhidi ya kituo cha polisi huko Sinai.

https://p.dw.com/p/15kTO
Mohamed Mursi, head of Muslim Brotherhood's political party, and Brotherhood's new presidential candidate, talks during interview with Reuters in Cairo.
Präsidentschaftswahl in Ägypten Mohamed MursiPicha: Reuters

Rais wa Misri, Mohammed Mursi ameapa kulidhibiti tena eneo la Sinai kufuatia shambulio karibu na mpaka na Israel lililosababisha vifo vya walinzi 16. "Nimeviamuru vikosi vyetu vyote vya usalama, jeshi na polisi, kuchukua hatua za haraka kuwatia mbaroni waliohusika na shambulio hilo la kinyama," amesema rais Mursi kwenye hotuba yake aliyoitoa kupitia televisheni mapema leo. (06.08.2012)

Rais Mursi amesema tukio hilo halitapuuzwa na kwamba vikosi vya usalama vitayadhibiti kabisa maeneo yote ya Sinai. Kiongozi huyo aidha amesema waliohusika watawajibishwa pamoja na washirika wao, iwe ni ndani au nje ya Misri.

"Hakuna nafasi kwa uhalifu wa aina hii katika jamii yetu. Kila mtu ataona kuwa vikosi vya usalama vya Misri, jeshi na polisi, vina uwezo wa kuwakata waliofanya shambulio hili popote walipo," ameongeza kusema rais Mursi.

Shambulio la jana dhidi ya kivuko cha Abu Salem kaskazini mwa Sinai kwenye mpaka kati ya Misri na Israel, lilitokea wakati wanaume waliokuwa na bunduki walipojaribu kuvuka mpaka kuingia Israel. Washambuliaji hao waliiba magari mawili ya jeshi la Misri yaliyokuwa na silaha waliyoyatumia kukivamia kivuko hicho, lakini moja likalipuka lilipokaribia mpaka wa Israel.

Duru za usalama nchini Misri zimesema ndege ya kivita ya Israel ililishambulia gari la pili katika kivuko cha Kermes Shalom kuelekea kusini mwa Gaza, eneo ambapo mipaka ya Israel, Misri na Gaza hukutana. Wanamgambo watano waliuwawa na maiti zao zimepatikana leo na jeshi la Israel.

Mtihani wa kidiplomasia

Shambulio hilo ni mtihani mgumu wa mapema wa kidiplomasia kwa rais Mursi tangu alipoingia madarakani mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu. Huenda pia likavuruga mahusiano kati ya Misri na chama cha Hamas kinachoutawala Ukanda wa Gaza, na ambacho kina mafungamano ya karibu na chama cha Udugu wa Kiislamu cha rais Mursi.

Rais Mursi aliitisha kikao cha dharura na maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Misri na kuapa kuchukua hatua kali baada ya shambulio hilo. "Waliouwawa kwenye shambulio hili wakati walipokuwa wakifuturu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, mashahidi hao, damu yao haijamwagika bure," amesema rais Mursi.

Wanamgambo wa Gaza watuhumiwa

Shirika la habari la serikali ya Misri limemnukuu afisa wa usalama akisema shambulio hilo limefanywa na wanamgambo walioingia Gaza kupitia njia ya chini ya ardhi pamoja na wanamgambo wengine kutoka maeneo mawili ya Sinai.

Chama cha Hamas kimesema kinachunguza shambulio hilo na hakina taarifa zinazoonyesha washambuliaji walitokea Gaza. Hata hivyo msemaji wa serikali ya Hamas, Taher al-Nono, amesema serikali inazifunga mara moja njia zote za chini ya ardhi katika mpaka na Misri.

Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak
Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud BarakPicha: AP

Waziri wa ulinzi wa Israel, Ehud Barak, ameitaka Misri ichukue hatua madhubuti kuepusha ugaidi katika eneo la Sinai. Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa upande wake ameipongeza hatua ya kishujaa ya jeshi la nchi hiyo na shirika la ujasusi, Shin Beit, kwa kutibua shambulio kubwa lililonuiwa kufanywa dhidi ya raia wa Israel.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri: Saumu Mwasimba