Misri yaingia tena kwenye mgogoro
30 Juni 2013Vuguvugu la Tamarod, jina la Kiarabu linalomaanisha uasi, ndilo linaloendesha kampeni ya kumng'oa Rais Mursi likidai kuwa limeshakusanya saini milioni kadhaa zinazounga mkono kampeni yao na kuitishwa uchaguzi mpya.
Mabango yanayowataka watu wajiunge na maandamano dhidi ya Mursi yameenea kila kipembe cha mji mkuu, Cairo, yakiwa yamebandikwa kwenye kuta na vioo vya magari pamoja na michoro ya "Juni 30."
Kuelekea maandamano ya leo, tayari watu wanane wameshauwa ndani ya wiki moja tu, akiwemo raia mmoja wa Marekani, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa kutoka pande zote mbili za waandamanaji.
Mursi, kiongozi wa ngazi za juu wa kundi la Udugu wa Kiislamu, ni rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, akiwa ameingia madarakani kupitia wimbi la mageuzi la mwaka 2011 kwenye nchi za Kiarabu, ambalo lilimaliza miongo mitatu ya utawala wa kidikteta.
Mursi atuhumiwa "kuyasaliti" mapinduzi
Wapinzani wake, waliopiga kambi nje ya kasri ya rais na uwanja wa Tahrir mjini Cairo, wanamtuhumu kwa kuyasaliti mapinduzi ya umma na kuyalimbikiza madaraka kwenye mikono ya Waislamu wenye siasa kali.
Lakini kwa upande mwengine maelfu ya wafuasi wake walikusanyika kwenye mji wa jirani wa Nasr kusikiliza hotuba kali zinazowataka kumlinda rais huyo.
Chama cha Uhuru na Haki, ambacho ni tawi la kisiasa la kundi la Udugu wa Kiislamu, kiliitisha "uhamasishaji mkubwa" katika kumuunga mkono Rais Mursi, ambaye amesema anataka kubakia madarakani hadi mwishoni mwa muhula wake, Juni 2016.
Lakini kiongozi mkuu wa upinzani, Mohammed el-Baradei, amemtaka Rais Mursi "kuwasikiliza watu" na kuondoka madarakani.
Hisia kali zinazooneshwa na pande zote mbili zinazopingana kwenye mgogoro huu, zinaelezea kwa kiasi gani jamii imegawanyika ndani ya taifa hilo lenye watu wengi zaidi kwenye ulimwengu wa Kiarabu.
Jeshi kuingilia kati
Jeshi, ambalo lilibeba jukumu kubwa baada ya mapinduzi yaliyomng'oa Hosni Mubarak, limeonya kwamba litaingilia kati endapo kutakuwa na machafuko makubwa.
Tangu kuingia madarakani, Mursi amekuwa akipambana na mahakama, vyombo vya habari na polisi, huku uchumi ukiwa umedumaa na uwekezaji kukauka kabisa na gharama ya maisha ikizidi kupanda juu.
Wamisri wamekuwa wakiweka akiba kubwa ya chakula na kutoa fedha zao kutoka benki, wakihofia maandamano ya leo. Tayari kumeripotiwa uhaba mkubwa wa mafuta ambao umesababisha misururu mikubwa ya magari na kuidumaza sehemu kubwa ya mji mkuu.
Kiasi cha wabunge wanane walijiuzulu siku ya Jumamosi wakiwaunga mkono waandamanaji wanaompinga Mursi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo