1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mitandao ya kijamii kushiriki uchaguzi Zambia

19 Septemba 2011

Wakati Wazambia wanapiga kura tarehe 20 Septemba, watakuwa na timu ya waangalizi makini kufuatilia mchakato huo, kupitia mitandao ya kijamii, ambamo wanaweza kuripoti makosa na ukiukaji wa taratibu katika uchaguzi huu.

https://p.dw.com/p/12cCE
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Zambia wa mwaka 2011.
Kampeni za uchaguzi mkuu wa Zambia wa mwaka 2011.Picha: picture alliance/ZUMA Press

Mpango uliopewa jina la Bantu Watch umezinduliwa hivi karibuni na jamii ya kiraia kuhakikisha taifa hilo la kusini mwa Afrika linakuwa na kiwango kikubwa cha ushiriki wa kiraia katika kusimamia uchaguzi.

Mfumo wake ni rahisi ambapo watu wanaweza kutuma ujumbe bila ya kujitambulisha kwa nambari ya ndani ya nchi 3,018 kwa kutumia simu za mkononi au wanaweza kuingia katika mtandao (www.bantuwatch.org) kuripoti visa vinavyotokea.

Waangalizi wa uchaguzi wa zamani walioko katika maeneo yanakotokea ripoti hizo, kwanza watayakinisha ukiukaji wa taratibu za uchaguzi unaohitaji kuchukuliwa hatua aidha na wafanya kazi wa uchaguzi au polisi.

Wakati wapiga kura watakapopiga kura Jumanne hii kumchaguwa rais, bunge na wawakilishi wa serikali za mitaa, kuna hofu ya kuzuka ghasia. Vyama vya upinzani vimekituhumu chama tawala cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) cha Rupiah Banda kwa kuwatishia wale wanaompinga rais na chama chake.

Maberegamu yenye picha za wagombea kwa uchaguzi mkuu wa Zambia wa mwaka 2011.
Maberegamu yenye picha za wagombea kwa uchaguzi mkuu wa Zambia wa mwaka 2011.Picha: picture alliance/landov

Jamii ya kiraia na wanasiasa wanaupongeza mpango huo na wanauona kuwa njia ya kushughulikia kwa haraka visa vyovyote vile.

SACCORD ni kituo cha Kusini mwa Afrika kinachoshughulikia utatuzi wa mizozo, huu ni mradi unaoendeshwa na jamii ya kiraia nchini Zambia na wawakilishi wa mtandao wa kijamii walioko chini ya kituo hicho.

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Lee Habasonda, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba huo ni utaratibu mzuri wa kuzuwiya ukiukaji wa taratibu za uchaguzi, kwa vile watu watakuwa wanaweza kuripoti kwa wakati unaotakiwa, mathalan makosa kama vile ya vitisho, hotuba za kuchochea chuki, kununuwa kura, upendeleo unaofanywa na makarani wa uchaguzi, upotoshaji wa habari za uchaguzi na kadhalika.

Hata wale wanaowania nafasi katika uchaguzi huo wameukaribisha mpango huo. Mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha National Restoration, Elias Chipimo Jr., amesema juhudi zozote zile ambazo zinaweza kusaidia kupunguza ghasia za uchaguzi zinapaswa kukaribishwa.

Amesema kumekuwepo na ghasia nyingi na vitisho kabla ya uchaguzi huu na juhudi zozote zile kuzuwiya hali hiyo hazitopuuzwa. Kwa mujibu wa Chipimo Jr., mmojawapo wa wanachama wao anauguza jeraha baada ya kushambuliwa na kada wa chama tawala na kwamba kuna mashahidi wanaoweza kuthibitisha jambo hilo.

Wapiga kura nao pia wanakaribisha juhudi hizo.

Tayari mtandao wa Bantu Watch umeanza kupokea habari kutoka nchini kote zenye kuelezea visa vya hongo, udanganyifu wa uchaguzi na ukiukaji wa kanuni za uchaguzi.

Repoti moja kutoka mtu aliejitambulisha kwa jina la "MSimushi" kutoka Senanga, magharibi ya Zambia, inasema: " Mawakala wa chama tawala cha MMD huko Senanga wako mbioni kujaribu kuwahonga wafanyakazi waliochaguliwa kusimamia uchaguzi kwa fedha taslimu ili wakipendelee chama hicho wakati wa kuhesabu kura"

Mwengine anasema" Uchaguzi wa Zambia: Magari yanayodaiwa kuwepo katika kampeni ya chama cha United Party for Development yalikuwa mali ya mahakama"

Mgombea wa chama tawala cha Zambia, MMD, Rupiah Banda.
Mgombea wa chama tawala cha Zambia, MMD, Rupiah Banda.Picha: dapd

Inatarajiwa watu wengi watawasiliana na mtandao huo wa Bantu Watch kutokana na kuwa rahisi kwa kile mtu anachotakiwa kufanya na hauhitajiki utaalamu mgumu wa kiufundi. Mtu anachotakiwa kufanya ni kutumia aidha simu ya mkono au mtandao ambayo ni majukwaa yanayotumiwa na watu wengi kila siku.

Habasonda, mkuu wa kituo cha SACCORD, anasema wasimamizi waliopatiwa mafunzo katika majimbo tisa nchini humo watayakinisha taarifa hizo za wananchi kabla ya kuziwasilisha kwa wahusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Akiunga mkono juhudi hizo mtaalamu wa vyombo vya habari katika Idara ya Mawasiliano na Umma, Chuo Kikuu cha Zambia, Dr. Elijah Mwewa Mutambanshika Bwalya amesema huo ni mpango mzuri wa hatimae kuwapa wananchi sauti katika mchakato wa kura licha ya kuwa na wasi wasi kwamba wale walioko vijijini hawatoweza kutumia Bantu Watch kwa vile wengi wao hawana simu za mkononi sembuse mtandao.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS
Mhariri: Miraji Othman