1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mitchell-Israel na Palestina

29 Januari 2009

Mjumbe wa Obama azungumza na viongozi wa Israel

https://p.dw.com/p/GiSc
G.Mitchell-Mjumbe wa ObamaPicha: AP / DW

Mjumbe wa Rais Barack Obama kwa Mashariki ya Kati,George Mitchel ameahidi kusukuma mbele kwa nguvu utaratibu wa amani kati ya Israel na wapalestina.Amedai wapiganajai wa mwambao wa Gaza wakomeshe kuingiza silaha huko kimagendo na mipaka iliofungwa na kuuzingira mwambao wa Gaza ifunguliwe ikiwa mpango wa kuacha mapigano udumu.

Bw.Mitchell amekuwa na duru ya kwanza ya mazungumzo na viongozi wa Mashariki ya Kati ili kuamua hatua gani utawala wa Rais Obama uchukue ili kuzifufua juhudi za amani kufuatia hujuma kali za Israel katika Mwambao wa Gaza.

Mjumbe wa Rais Obama George Mitchell amesema baada ya mazungumzo yake na waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel mjini Jeruiselem:

"Mimi na waziri mkuu, tumezungumza kwamba , kuimarishwa mpango wa kusimamishwa mapigano, ndio muhimu kabisa pamoja na kukomesha kabisa uchokozi, kuingizwa silaha kimagendo na kufunguliwa mipaka ya kuingilia Gaza kwa muujibu wa mapatano ya 2005."

Bw.Mitchell hapo akigusia yale mapatano yanayodai kivuko cha mpakani cha Rafah,mpakani mwa gaza na Misri-mpaka pekee usiogandana na Israel ambayo yalikuwa yasimamiwe kati ya vikosi vya Misri na vya Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina pakiwepo pia wachunguzi wa Umoja wa Ulaya na ukaguzi wa Israel kupitia mitambo ya kamera.

Hatahivyo, wapiganaji wa kipalestina walifyatua mapema leo asubuhi makombora ndani ya Israel na Jeshi la Israel nalo likaarifu kuwa ndege zake za kivita zimehujumu njia za chini kwa chini za kupenyezea silaha kimagendo pamoja na kiwanda cha silaha huko Gaza.

Bw.Mitchell alikutana jana na viongozi wa Israel baada ya kuwasili Jeruselem akitokea Misri akiwa katika hatua yake ya pili ya ziara yake ya Mashariki ya Kati ya kutimiza utumwa aliopewa na Rais barack Obama wa kufanya juhudi kubwa kuufufua utaratibu wa amani kati ya waisraeli na wapalestina.

Akirejea matamshi aliotoa Misri baada ya mkutano wake na Rais Hosni Mubarak,Bw.Mitchell aliahidi kuwa "Marekani itaseleleza juhudi imara zenye yshabaha ya kufikia kuundwa kwa dola 2 -ile ya waisrael na ya wapalestina zikiishi bega kwa bega kwa amani na katika hali ya usalama."

Bw.Mitchell akaongeza na ninamnukulu,

"Uamuzi wa Rais Obama kunituma katika eneo hili hata haikupita wiki tangu kutawazwa rais ni ushahidi dhahiri-shahiri ya nia yake ya dhati." Alisema Mitchell huko Cairo kabla kuwasili jana Jeruselem.

Waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel, alisema Israel itaifungua mipaka ya Gaza ambayo imeifunga kupita kila kitu isipokuwa bidhaa na shehena muhimu tangu chama cha kiislamu cha Hamas kunyakua madaraka huko Gaza Juni,2007,ikiwa tu wapiganaji wa Hamas wakimuacha huru mwanajeshi wa Israel waliomnyakua hapo juni,2006.

"Kufunguliwa kwa njia ya ,kudumu kwa mipaka ya kuingilia Gaza kutafungamanishwa na swali la hatima ya Gilad Shalit." -mjumbe wa hadhi ya juu wa Israel alinukuliwa kusema.

Ziara ya Bw.Mitchell katika Mashariki ya Kati, imekuja katika hali ya kuripuka tena kwa machafuko kandoni mwa Gaza tangu Januari 18 pale Israel, ilipositisha hujuma zake za siku 22 katika shina la Hamas.

Wapiganaji wa kipalestina nao, walimuua jana askari-jeshi wa Israel katika mripuko wa bomu karibu na mpakani; na Israel haikukawia kulipiza kisasi kwa kushambulia kwa mizinga iliomuua mkulima mmoja wa kipalestina na hujuma za anga zilizowajeruhi wengine 3 na hujuma nyengine katika njia za chini ya ardhi. Mapatano ya kusimamisha mapigano huko Gaza kwa sasa yanaendelea alao kwa jina tu.