Mjadala kuhusu ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za ACP mjini Bonn
13 Machi 2007Mjadala huo rasmi kati ya mawaziri wa misaada ya maendeleo wa umoja wa ulaya na karibu mawaziri 30 wa kundi la nchi za Afrika, Caribbean na Pasifik-ACP ulifunguliwa jana usiku mjini Bonn na waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Bibi Heidemarie Wieczorek-Zeul. Mkusanyiko huo ni katika lile jukwaa la mikutano ya mawaziri wa umoja wa Ulaya.
Zingatio la Ujerumani kama mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya ni masuala yanayohusika na sera ya maendeleo. Hayo ni pamoja na mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi pamoja na nchi za Afrika, Carribean na eneo la Pasifik, kundi linalojulikana kama ACP, nishati kwa Afrika, maendeleo ya nishati mbadala, haki na usawa katika masuala ya ajira katika sera ya maendeleo ya Ulaya na utaratibu wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na eneo la maziwa makuu.
Kumekuweko na mvutano mkubwa baina ya Umoja wa ulaya na mataifa ya ACP kuhusu mapendekezo ya mikataba ya ushirikiano, ambayo inapaswa kusainiwa na ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Mawaziri wa nchi za ACP wamependekeza mbele ya Umoja wa ulaya kuweko na makubaliano ya muda hadi Januari 2008, wakidokeza kwamba kuna hatari kuwa muda uliowekwa wa majadiliano hautofikiwa, kukiwa na wasi wasi kwamba nafuu na ridhaa katika sekta ya forodha kwa bidhaa zinazotoka katika nchi za ACP , muda wake utafikia kikomo. Wachambuzi wanaamini kwamba ikiwa mikataba ya ushirikiano haitosainiwa ifikapo mwisho wa mwaka, kuatakuweko na maridhiano ya kurefusha muda.
Akizungumza na waandishi habari kabla ya ufunguzi wa mkutano huo wa Bonn kati ya mawaziri umoja wa Ulaya na nchi za ACP, waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Bibi Wieczorek-Zeul alisema,“Hatujadiliani na wala si Ujerumani ikiwa kama mwenyekiti, na ningesema wazi kwamba mawaziri wa misaada ya maendeleo wa umoja wa Ulaya wana azma ya kuona kuna muelekeo wa maendeleo kupitia mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi. Hapana budi pia juhudi za maendeleo ziwekwe usoni. Na msimamo wangu wakati wote ni kwamba kuwepo na tarehe kwa mfano kama sehemu moja, lakini pia pengine kuwe na uwezeaano wa kuwa na kifungu maalum ambapo akatika kipindi fulani kutafanywa tathimini ya mikataba ya Ushirikiano. Huo unaweza kuwa uwezeakno mmoja wapo.”
Jana usiku mjadala kati ya pande hizo mbili ulianza kwa kushiriki pia rais wa Benki ya dunia Paul Wolfowitz, pakijadiliwa suala la vitega uchumi na uwekezaji barani Afrika na haja ya kukua uchumi, ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia katika bara hilo. Bw Wolfowitz aliyewasili Bonn akitokea ziarani katika baadhi ya nchi za Afrika, alikua na mtazamo wa matumaini kuhusika na mikataba ya ushirikiano wa kiuchum,“Kwa wakati huu, ningesema kwamba kuna nchi nyingi za kiafrika zinazofanya vizuri, na zinachohitaji ni msaada mdogo tu wa fedha. Kuna mambo mengine pia. Hakuna sekta ya binafsi bila ya umeme na barabara.”
Kwa upande wake naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Dr Asha Rose Migiro, aliyealikwa kama mzungumzaji, alisema kabla ya kikao hicho kwamba ,“Ninafikiri kuwa Umoja wa ulaya hauna budi kushirikiana na nchi za ACP, kukabiliana na changa moto za maendeleo zinazolikabili bara hilo kwa wakati huu. Rais wa Benki ya dunia amezungumzia miundo mbinu-Hiyo ni changa moto kubwa kwa hivyo ninafikiri kama Umoja wa ulaya utashirikiana na nchi hizi katika nyanja hizo, itakua hatua moja mbele katika kufuta umasikini barani Afrika.”
Masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo wa Bonn, kati ya Umoja wa ulaya na nchi za ACP, yatawasilishwa katika mkutano rasmi wa mawaziri wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya tarehe 12 na 13 ya mwezi wa Mei.