1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Paris kutangaza tahadhari ya juu dhidi ya COVID-19

5 Oktoba 2020

Maafisa nchini Ufaransa wanatarajiwa kutangaza leo tahadhari ya hali ya juu katika mji wa Paris na viunga vyake kuhusu wimbi jipya la mripuko wa corona. Kwingineko huenda Rais Trump akaruhusiwa kuondoka hospitalini.

https://p.dw.com/p/3jRdH
Frankreich I Coronavirus | Menschen mit Mundschutzmasken am Eiffelturm
Picha: Charles Platiau/Reuters

Nchini Marekani, Rais Donald Trump ambaye amelazwa hospitalini akitibiwa ugonjwa wa COVID-19 ameonekana akiwa ndani ya gari lake nje ya hospitali akiwapungia mkono wafuasi wake, huku madaktari wake wakisema anaweza kuondoka hospitali leo. 

Likimnukuu Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex, shirika la habari la Ufaransa AFP liliripoti usiku wa kuamkia leo kwamba miongoni mwa masharti ambayo huenda yatatangazwa mjini Paris ni kufunga migahawa pamoja na tahadhari zaidi za kuzingatiwa dhidi ya COVID-19.

Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa meya wa mji mkuu wa Paris Anne Hidalgo atatangaza mikakati hiyo mipya leo, na itatekelezwa kwa muda wa siku 15.

Soma pia: Ufaransa na Uingereza zashuhudia ongezeko la corona

Wiki iliyopita, waziri wa Afya wa Ufaransa Olivier Veran alitangaza mikakati mipya ya kuzuia kuzuka kwa maambukizi zaidi ya virusi vya corona, ikiwemo kufunga mabaa.

Hapo jana, Ufaransa ilirekodi maambukizi mapya ya juu ya watu 16,972. Tangu janga la corona lianze, zaidi ya watu 32,000 wamefariki kutokana na virusi hivyo nchini Ufaransa.

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Johanna Geron/AP Photo/picture-alliance

Ursula von der Leyen ajiweka karantini

Hayo yakijiri, rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, ametangaza kuwa amejiweka karantini baada ya kukaribiana na mtu aliyeambukizwa virusi vya corona.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, amesema alishiriki kwenye mkutano Jumanne iliyopita, ambao pia ulihudhuriwa na mtu aliyepimwa jana na kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya corona. Von der Leyen amesema mwenyewe alipimwa siku ya Alhamisi na hakuwa na virusi hivyo, lakini atafanya vipimo vingine tena leo.

Wiki iliyopita von der Leyen alihudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwa siku mbili.

Rais Trump alipewa tiba ya 'steroid' baada ya viwango vya oksijeni katika damu kushuka mara mbili

Rais Donald Trump akiwapungia wafuasi wake mkono akiwa ndani ya gari lake nje ya hospitali ya Walter Reed
Rais Donald Trump akiwapungia wafuasi wake mkono akiwa ndani ya gari lake nje ya hospitali ya Walter ReedPicha: Alex Edelman/AFP/Getty Images

Katika tukio tofauti, Rais Donald Trump wa Marekani ambaye anatibiwa dhidi ya COVID-19 katika hospitali ya taifa na ya kijeshi Walter Reed nchini humo, jana alionekana ndani ya gari lake nje ya hospitali hiyo akiwapungia mkono wafuasi wake.

Kitendo ambacho kinakiuka tahadhari ambazo zimewekwa kudhibiti virusi hivyo ambavyo vimesababisha alazwe hospitalini na ambavyo pia vimeshawaua zaidi ya watu 209,000 nchini mwake pekee.

Soma pia: Trump asema siku za karibuni zitakuwa muhimu kuekelea kupona

Baadhi ya wataalamu wa afya nchini Marekani wameishutumu hatua ya Trump kuondoka hospitalini kwa gari kuwapungia wafuasi wake.

Awali, timu ya madaktari wake ilisema viwango vya oksijeni katika damu yake vilishuka ghafla mara mbili katika siku za hivi karibuni, na kwamba walimpa tiba aina ya "steroid”, ambayo hushauriwa tu kupewa wagonjwa ambao wako mahututi.

Licha ya hayo, madaktari wa Trump walisema afya yake inazidi kuimarika na anaweza kuruhusiwa kuondoka hospitalini leo Jumatatu.

Mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni, Papa Francis
Mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni, Papa FrancisPicha: Vatican Media/Reuters

Papa Francis: Ipo haja kwa aina mpya ya siasa inayokuza mazungumzo na ushirikiano

Kwenye tukio jingine, mkuu wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis amesema janga la corona limethibitisha kuwa yale yanayotajwa kuwa "nadharia za kimiujiza” za masoko ya kibepari zimeshindwa, na kwamba ulimwengu unahitaji aina mpya ya siasa inayokuza mazungumzo na ushirikiano na inayopinga vita kwa njia zote.

Hapo jana Papa Francis aliweka wazi maono yake ya baada ya COVID-19 ya kuunganisha mambo ya msingi ya mafundisho yake kuwa waraka mpya kwa maaskofu wote.

Mtindo wa nywele wa 'corona' Kenya

Idadi ndogo yajitokeza kuandamana dhidi ya taratibu za kupambana na COVID-19 Ujerumani

Kando na hayo, takriban watu elfu moja walishiriki misa kanisani na pia kuandamana kupinga taratibu ambazo zimewekwa na serikali ya Ujerumani kukabili virusi vya corona.

Maandamano hayo yalifanyika kwa siku ya pili katika mji wa mpakani wa Ujerumani Konstanz jana Jumapili. Hata hivyo idadi ya watu waliojitokeza ilikuwa chini kuliko idadi iliyotarajiwa ya kati ya watu 3,500 hadi 4,000.

(AFPE,DPAE, APE)