1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkanganyiko juu ya vyombo habari vilivyofunguliwa Tanzania

Hawa Bihoga8 Aprili 2021

Licha ya maagizo ya Rais Samia Hassan kuhusu vyombo vya habari vilivyofungiwa nchini Tanzania kuruhusiwa, mkanganyiko wa tafsiri juu ya maagizo hayo bado unaendelea kutamalaki.

https://p.dw.com/p/3rjak
Tansania Dodoma | Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: Habari Maalezo

Watendaji wa wizara inayohusika na habari imejaribu kutofautisha kati ya vyombo vinavyotakiwa kufunguliwa na visivyoruhusiwa. Wadau wa sekta hiyo wameitaka wizara hiyo kuacha kupotosha maagizo ya rais. 

Ni hali inayoweza kuelezwa kama shagala baghala au soko moko la aina yake kwa watendaji wakuu wa wizara ya habari, ambao licha ya maagizo ya rais kuwa wazi kabisa, wamekuja na maelezo yanayoonekana kuwakanganya zaidi wamiliki wa vyombo vilivyofungiwa na hasa magazeti. Magazeti ya Mwanahalisi na Mawio, ambayo licha ya kumaliza adhabu yake na kushinda kesi mahakamani, bado wizara haijarejesha leseni ya vyombo vyake.

Katibu mkuu wizara y amasuala ya habari katibu Hassan Abbas. (Picha ya maktaba)
Katibu mkuu wizara y amasuala ya habari katibu Hassan Abbas. (Picha ya maktaba)Picha: Deo Makomba/DW

Waziri anayeshughulikia masuala ya habari Innocent Bashungwa na katibu mkuu wake Hassan Abbas, walisema kauli ya rais Samia Suluhu Hassan ilikuwa inahusu vyombo vya habari vya kidigitali tu, na kuwataka wamiliki wa magazeti yaliyofungiwa kwenda wizarani kujadili vifungu vilivyotumiwa kuwafungia.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania Kajubi Mukajanga, ameshauri wamiliki hao waende kujadiliana na wizara, lakini amesisitiza kuwa mkanganyiko unaoshuhudiwa sasa unashadidiwa na sheria kandamizi zilizotungwa kwa lengo la kuminya uhuru wa habari.

Wito watolewa wamiliki wa vyombo vilivyofungiwa kushauriana na serikali
Wito watolewa wamiliki wa vyombo vilivyofungiwa kushauriana na serikaliPicha: DW/E. Boniphace

Wakati wa shughuli ya kuwaapisha makatibu wakuu, manaibu wao na watendaji wakuu wa taasisi za serikali mapema wiki hii, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa agizo kwa vyombo vya habari vilivyofungia kufunguliwa, na kuviita vyombo hivyo kuzingatia sheria na maadili. Lakini majibu yaliyotolewa na watendaji wa wizara yameacha maswali mengi juu ya uelewa wao wa agizo hilo la Rais.

Sekta ya habari ni mojawapo ya zilizokabiliwa na wakati mgumu sana wakati wa utawala uliyopita, ambapo vyombo kadhaa vilifungiwa na vingine kulaazika kujikagua vyenyewe ilikuepuka rungu la serikali.