1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Mkasa wa moto wauwa watu 82 nchini Iraq

25 Aprili 2021

Zaidi ya watu 80 wamekufa baada ya moto kuzuka kwenye hospitali ya wagonjwa wa Covid-19 nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/3sY7K
Irak | Corona-Intensivstation | Mehr als 20 Tote bei Brand in Krankenhaus in Bagdad
Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Tukio hilo limesababisha hasira miongoni mwa raia wa taifa hilo na kupelekea kufutwa kazi kwa maafisa wa ngazi ya juu wa serikali kwenye taifa hilo ambalo miundombinu yake ya afya imechakaa na mikongwe.

Wengi ya wahanga walikuwa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua na walikosa hewa kutokana na moshi mzito au kuungua wakati moto ulipozuka kwenye hospitali ya Ibn al-Khatib Mashariki ya mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Duru zimesema moto huo ulizuka baada ya kutokea mlipuko uliosababishwa na hitilafu kwenye ghala la kuhifadhi mitungi ya gesi ya Oksijeni

Wizara ya afya imesema watu 82 wamekufa na wengine 110 wamejeruhiwa huku tume ya haki za binadamu nchini Iraq ikisema watu 28 miongoni mwa waliopoteza maisha ni wagonjwa waliolazimika kutolewa kwenye mashine za kuwasaidia kupumua ili kuokolewa kutoka kwenye mkasa huo.

Moto huo ulisambaa haraka kwenye ghorofa kadhaa usiku wa manane hususan kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi ambako wengi ya watu wenye hali mbaya wanatibiwa.

"Hospitali haikuwa na mfumo wowote wa kuzuia moto na mbao dhaifu kwenye dari zilifanya iwe rahisi kwa moto kusambaa haraka kwenye vitu vinavyoshika moto kwa urahisi" Asasi ya huduma za kiraia nchini Iraq imesema kwenye taarifa yake.

Waziri wa afya afutwa kazi kufuatia ajali ya moto

rak | Corona-Intensivstation | Mehr als 20 Tote bei Brand in Krankenhaus in Bagdad
Picha: Murtadha Al-Sudani/AA/picture alliance

Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhemi amemtimua kazi waziri wa afya Hassan al-Tamimi - ambaye anaungwa mkono na kiongozi wa kidini mwenye nguvu Moqtada al Sadr.

Kutimuliwa kwake kunafuatia miito kwenye mitandao ya kijamii ya kutaka aondolewe kazini kupisha uchunguzi ambao utamjumuisha pia gavana wa mji wa Baghdad.

Waziri Mkuu Khademi pia ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa huku bunge likisema litatumia mkutano wake wa siku ya Jumatatu kuhani msiba huo.

Walioshuhudia wamesema zoezi la uokoaji lilikwenda taratibu na bila mpangilio huku wagonjwa na ndugu zao walisongamana kwenye ngazi wakijaribu kujinusuru.

"Ni raia ndiyo waliowatoa waliojeruhiwa nje ya jengo" amesema Amir kuliambia shirika la habari la AFP akisimulia jinsi alivyonusurika wakati akiwaokoa kaka zake waliokuwa wamelazwa.

Mifumo ya afya ya Iraq ni mikongwe 

Irak | Corona-Intensivstation | Mehr als 20 Tote bei Brand in Krankenhaus in Bagdad
Picha: Thaier Al-Sudani/REUTERS

Hospitali nyingi nchini Iraq zipo kwenye hali mbaya kutokana na miongo kadhaa ya vita na uwekezaji duni huku nyingi hazina dawa wala vitanda.

Hata hivyo wengi lakini wanalaumu ukosefu wa umakini na tabia ya rushwa iliyokita mizizi kama chanzo cha ajali hiyo ya moto.

"Balaa hili kwenye hospitali ya Ibn al-Khatib ni matokeo ya miaka chungunzima ya kumomonyoka kwa taasisi za taifa kutokana na rushwa na uendeshaji mbovu" ameandika rais Barham Saleh wa Iraq kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Mkasa huo wa moto umesababisha hasira ya umma kupitia mitandao ya kijamii. Gavana wa mji wa Baghdad Mohammed Jabir amependekeza   wizara ya afya iunde tume ya uchunguzi ili wote amabo hawakutimiza wajibu wafikishwe mbele ya vyombo vyas sheria.