Mkataba wa kudhibiti silaha wapitishwa
3 Aprili 2013Hatua hii imeafikiwa baada ya kampeni ya zaidi ya muongo mmoja ya kutaka kuzuia silaha zisiangukie katika mikono ya magaidi, wahalifu na wale wanaotaka kuhujumu haki za binaadamu.
Baada ya tangazo hilo kwamba mkataba wa kimataifa wa kudhibiti silaha umepitishwa kulisikika sauti za kufurahia swala hilo. Bao la elektroniki lililokuwa mbele ya mkutano huo lilionesha matokeo ya kura zilizopigwa.
Takriban nchi 153 kati ya 193 zilipigia kura mkataba huo huku nchi tatu zikiupinga na nyengine 23 zikiamua kutoupigia kura kabisa mkataba huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema, kupita kwa mkataba huo ni ushindi kwa watu duniani kote.
Ban amesema mkataba huo wa kudhibiti biashara ya mabilioni ya fedha ya silaha utatoa changamoto kubwa kwa wanaotaka kupitisha silaha hizo kwa njia haramu.
Iran, Korea Kaskazini na Syria wapinga Mkataba
Hata hivyo Marekani ambaye ndio mfanyibiashara mkuu wa silaha hizi pia imeridhia mkataba huo. Iran, Korea Kaskazini na Syria wote wanaokumbwa na vikwazo vya silaha waliupigia kura ya hapana.
Nchi hizo zimesema mkataba huo wa kudhibiti biashara ya silaha unaipendelea Marekani ambayo ni mfanyabiashara mkubwa na kuwapokonya wao haki ya kuingiza silaha nchini mwao kwaajili ya kujilinda.
Korea Kaskazini kupitia Naibu Balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa Ri Tong Il amesema kuna hatari kubwa ya kutumia vibaya mamlaka ya kisiasa na kuingiliwa kwa maswala ya ndani ya nchi.
Nchi tano kubwa za biashara ya silaha duniani ni Marekani, Urusi, Ujerumani, Ufaransa na China. Kwa upande wao Urusi na China ambao pia ni wafanyabiashara wakubwa wa silaha walisusia kupigia kura mkataba huo.
India na Indonesia pamoja na mataifa mengi ya kiarabu kama Misri, Saudi Arabia, Sudan na Qatar, pia wakachukua njia hiyo hiyo huku nchi inayomiliki silaha za nyuklia kama Pakistan ikiuunga mkono.
Mkataba wa Kwanza wa kudhibiti silaha
Sasa nchi zote zitalazimika kuripoti mauzo yote ya silaha na hata kufanya uchunguzi juu ya pale silaha hizo zinapouziwa ili kuzuia silaha hizo kuingia mikononi mwa magaidi.
Hakujawahi kuwa na mkataba wa kimataifa unaodhibiti biashara ya silaha inayokadiriwa kuingiza kima cha dola bilioni 60 kwa sasa hatua ambayo shirika la Amnesty International linasema fedha zinazotokana na biashara hiyo huenda zikapanda na kufikia dola bilioni 100 kwa kipindi cha miaka 4 ijayo.
Frank Jannuzi Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Marekani amesema hatua iliopigwa leo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa imetoa nafasi ya moja kwa moja ya watu wanaotetea haki za binaadamu kusimama na kuendeleza wito wao huo kwa kuzuia silaha haramu kupitishwa kwa mataifa mengine na hii itasaidia pakubwa katika kulinda maisha ya raia wengi katika nchi mbali mbali.
Hata hivyo chama cha wamiliki bunduki nchini Marekani NRA kimeapa kupinga mkataba huo katika bunge la Marekani, wakisema kuwa hatua hii itahujumu haki za kumiliki silaha za nchi hiyo.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri Josephat Charo