Mkataba wa Lisbon wakiuka kizingiti muhimu Czech
7 Mei 2009Baraza la Senet la Jamhuri ya Czech limeidhinisha mkataba wa Lisbon na kwa namna hiyo kuondowa kizingiti kikubwa katika njia ya kukubaliwa mpango wa kufanyiwa marekebisho taasisi za Umoja wa Ulaya.Hata hivyo rais Vaclav Klaus anasema hatoidhinisha mkataba huo.
Baraza la Senet la jamhuri ya Czech limeidhinisha mkataba huo wa Lisbon kwa sauti 54 dhidi ya 20.
"Ni tukio muhimu kwa msimamo wa jamhuri ya Czech barani Ulaya na katika dunia" ameshangiria naibu waziri mkuu aliyejiuzulu wa Jamhuri ya Czech Alexandr Vondra,aliyeutetea sana mkataba huo bungeni February mwaka huu na hivi sasa katika baraza la Senet.
Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,José Manuel Barroso na wakuu wa makundi yote ya kisisa yanayowakilishwa katika bunge la Ulaya wameusifu uamuzi wa baraza la Senet la jamhuri ya Czech.
Hata hivyo utaratibu wa kuidhinishwa mkataba huo na jamhuri ya Czech,ambayo ndio mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya hadi mwishoni mwa mwezi July mwaka huu utakamilika tuu ikiwa rais Vaclav Klaus atatia saini.
Lakini tangu jana rais huyo ,mashuhuri kwa upinzani wake dhidi ya Umoja wa Ulaya ameshasema hatotia saini bado mkataba huo.Ameelezea msimamo wake huo kutokana na ile hali kwamba mwaka jana mkataba huo ulikataliwa na Ireland na zaidi ya hayo kuna wapinzani wa mkataba huo wanaopanga kutuma malalamiko yao katika mahkama ya katiba ya jamahuri ya Czech.Rais Vaclav Klaus anataka kusubiri anasema:
"Mkataba wa Lisbonne hauna maana yoyote wakati huu tulio nao.Hauna maana kwasababu umekataliwa na nchi mojawapo mwanachama.Hiyo ndio sababu kwanini sifikirii mie kuuidhinisha kwa sasa" amesema rais Vaclav Klaus na kuongeza:
"Kwanza kabisa nnabidi nielezea jinsi nilivyovunjika moyo kwa uamuzi uliopitishwa.Ni jambo la kusikitisha kushuhudia uzembe wa baadhi ya wanasiasa wetu.Kila mara wamekua wakitoa hoja za uwoga.Eti nchi yetu ni ndogo,dhaifu na haina maana yoyote barani Ulaya.Tunabidi kunyenyekea,hata kama hatukubaliani na hoja hizo.Mie napinga."
Rais Vaclav Klaus ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa mkataba wa Lisbon ambao kwa maoni yake unaipunguzia mamlaka nchi yake .
Uwezekano wa kukataliwa mkataba huo na jamhuri ya Czech ulizusha wasi wasi mjini Bruxellews hasa kwakua utaratibu wa kuidhinishwa mkataba huo umekua ukidorora tangu miezi kadhaa sasa barani Ulaya.
Ili kuishinikiza,baadhi ya nchi za umoja wa ulaya,ikiwemo Ufaransa na Ujerumani zilitishia kuzuwia utaratibu wa kupanuliwa umoja wa ulaya,uliowakaa sana wacheki.
"Sijaukubali kwa moyo mkunjufu mkataba wa Lisbon,lakini nnauangalia kama fidia tunayobidi kutoa ili kushiriki katika utaratibu wa kuungana Ulaya" alisema hayo waziri mkuu anaeacha wadhifa wake Mirek Topolanek kabla ya kura kupigwa katika baraza la Senet.
"Baada ya kuvunjika serikali yetu kati kati ya wadhifa wetu wa mwenyekiti wa Umoja wa ulaya,hatuwezi kuacha aibu nyengine itokee" ameshadidia.
'Hivi sasa litakua jukumu la serikali mpya ya mpito itakayokabidhiwa madaraka kesho ijumaa na kuongozwa na Jan Fischer, kuhakikisha utaratibu huo unakamilika.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Abdul Rahman