1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mke wa Assad naye awekewa vikwazo

23 Machi 2012

Umoja wa Ulaya umewawekea vikwazo vya kusafiri, na kuzuia mali zao zilizoko ndani ya nchi wanachama wa Umoja huo, jumla ya watu 12 wa karibu wa Rais Bashar Assad akiwemo Mkewe, Asma al Assad.

https://p.dw.com/p/14Q0O
Rais Bashar Assad na mkewe Asma
Rais Bashar Assad na mkewe AsmaPicha: dapd

Idadi hii inafanya watu waliyowekewa vikwazo nchini Syria na Umoja wa Ulaya kufikia 126 huku idadi ya makampuni ikiwa 39, yakiwemo mabenki na makampuni ya mafuta ambayo yanadaiwa kufadhili utawala wa rais Assad. Mei 23 mwaka jana Umoja huo ulimuwekea pia vikwazo rais Assad pamoja na maafisa wengine 9 wa ngazi ya juu.

Uturuki yaongeza shinikizo
Waziri wa Mambo ya nje wa Uturuki, Ahmet Davotoglu aliyehudhuria Mkutano huo, alisema taarifa iliyotolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuunga mkono juhudi za Mjumbe Maalum Koffi Annan isiangaliwe kama muda mpya kwa utawala nchini Syria kuendeleza mauaji, na kuongeza kuwa laazima hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton akizungumza na baadhi ya Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton akizungumza na baadhi ya Mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huoPicha: dapd

"Tunaendelea kudhani kuwa Syria inacheza na muda na laazima tufanye kitu kuhakikisha umuagaji damu unakoma. Ili kukomehsa janga hili la kibinadamu, laazima tusimame pamoja," alisema Davutoglu na kuongeza kuwa kupiga simu pekee hakutoshi.

Akizungumzia vikwazo hivyo, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton amesema; "Nadhani vikwazo hivi vinasaidia kuongeza shinikizo kwa utawala, hilo sina shaka nalo. Vikwazo vinaleta tofauti muhimu kwa sababu vinafanya mambo mawili: Moja ni kwamba vinalenga mtu au shirika mmoja mmoja katika hali inayowazuia kuendelea na maisha kama kawaida, na pili, vinatoa ujumbe mzito wa kisiasa"

Tume ya uchunguzi yaongezewa muda
Wakati huo huo Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limeongeza muda wa tume inayochunguza ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Syria na kuitaka tume hiyo iendelee kukusanya taarifa za ukiukwaji huu ambazo zitakuwa zinachapischwa mara kwa mara.

Tume hii iliyoundwa mwezi Februari ilikabidhi orodha ya majina wa maafisa wa serikali ya syria inaowashuku kushiriki vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. lakini balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa alipinga vikali ripoti ya tume hii na kusema kuwa imeegemea upande mmoja.

Annan azishawishi Urusi, China
Wakati huo huo, Mjumbe wa Umoja wa mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu katika mzozo wa Syria Koffi Annan leo anazitembelea nchini za China na Urusi kujaribu kuzishawishi ziunge mkono juhudi zake za kutatua mgogoro huo, ambao hadi sasa umegharimu maisha ya watu zaidi ya 9000 kwa mujibu wa mashirika ya uangalizi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssesanga\RTRE\DPAE\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman