1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkenya aivunja rekodi ya dunia ya marathon kwa wanawake

15 Oktoba 2024

Ruth Chepng'etich wa Kenya ameivunja rekodi ya dunia ya mbio za marathon kwa karibu dakika mbili katika mbio za Chicago Marathon, alipoibuka bingwa kwa muda wa 2:09:56 mnamo Jumapili.

https://p.dw.com/p/4lons
USA I Chicago - Ruth Chepngetich, Marathon-Weltrekord
Picha: Patrick Gorski/USA TODAY Sports/Reuters

Chepng'etich aliye na umri wa miaka 30 ameivunja rekodi iliyowekwa na Muethiopia Tigst Assefa aliyeweka rekodi ya 2:11:53 katika mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani.

Chepng'etich alikuwa na haya ya kusema baada ya mafanikio hayo.

Mwanariadha wa Kenya Ruth Chepng'etich
Mwanariadha wa Kenya Ruth Chepng'etichPicha: Patrick Gorski/USA TODAY Sports/Reuters

"Najihisi vizuri sana, ninajivunia na namshukuru Mungu kwasababu hii ilikuwa ndoto yangu. Nimepambana sana nikifikiria rekodi ya dunia na sasa nimelifanikisha hilo kwa hiyo nashukuru," alisema Chepng'etich.

Kwa upande wa wanaume Mkenya mwengine John Korir, aliebuka mshindi kwa saa 2:02:44 na kumshinda Muethiopia Mohamed Esa.

"Leo nilijihisi vyema sana kukimbia kwa saa mbili na dakika mbili na kuweka muda wangu bora zaidi na hatimaye kushinda marathon ya Chicago. Unajua unapokuja hapa, unachokifuata ni ushindi na wala si muda," alisema Korir.

Vyanzo: Reuters/AP/AFP