1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutanao wa kimataifa kuhusu Usalama Magazetini

Oumilkheir Hamidou
11 Februari 2019

Mkutano wa kimataifa kuhusu usalama mjini Munich, mzozo wa Venezuela na juhudi za kuyanusuru makubaliano ya kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, Brexit ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3D7Kx
Wolfgang Ischinger, Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: DW

Tunaanzia mjini Berlin ilikochapishwa ripoti kuhusu hali namna ilivyo kabla ya mkutano wa mwaka huu wa kimataifa kuhusu usalama utakaofanyika mjini Munich. Gazeti la "Volksstimme" linaandika: "Miaka mitano imepita tangu rais wa zamani wa shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Joachim Gauck alipohutubia mkutano wa kimataifa kuhusu usalama mjini Munich na kutoa wito wa kuzidi kuwajibika Ujerumani na Umoja wa Ulaya katika majukwaa ya kimataifa. Siku chache kabla ya mkutano wa mwaka huu wa 2019 kuhusu usalama kuitishwa, matokeo ya wito huo ni finyu. Umoja wa Ulaya umezidi kugawanyika. Ufaransa imemrejesha nyumbvani balozi wake kutoka Rome ikilalalamika baada ya viongozi wa Italia kuwaunga mkono wanaharakati wa vizibao vya manjano.

Uingereza inakurubia kujitoa katika Umoja wa Ulaya bila ya maridhiano. Licha ya juhudi za miaka miwili za waandalizi wa mkutano wa kimataifa kuhusu usalama, kumuomba kansela Merkel ahudhurie mkutano huo, kiongozi mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron anasema hatoshiriki. Nchi za Ulaya mashariki na pia Ufaransa zinahisi usalama wao haukuzingatiwa kutokana na mradi wa Ujerumani wa kupatiwa gesi ya Urusi mashuhuri kwa jina Nord Stream nambari mbili."

Makosa kuingilia mambo ya ndani ya nchi huru

Mvutano wa Venezuela unazidi makali. Spika wa bunge Juan Guaido anapimana nguvu na rais Nicolas Maduro akijivunia uungaji mkono wa mataifa yasiyopungua 40. Ujerumani ni miongoni mwa mataifa hayo. Hata hivyo mhariri wa gazeti la " Badische Neueste Nachrichten" linakosoa msimamo wa Ujerumani na kuandika: "Ujerumani imechukua msimamo mbaya kwa kuelemea upande wa rais wa mpito wa Venezuela Guaido. Kwamba mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya yamefuata mfano wa Ujerumani, haisaidii kitu. Uamuzi huo ni tete kwa sababu unakwenda kinyume na msingi wa nchi kuwa huru. Mwongozo wa Umoja wa mataifa na sheria za kimataifa zinakataza moja kwa moja mataifa ya kigeni kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine."

Maridhiano yaafikiwe kuhusu Brexit

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha katika njia panda inayoziunganisha Uingereza na Umoja wa Ulaya. Gazeti la Donaukurier linamulika kasheshe ya kujitoa Uingereza katika Umoja huo - au Brexit na kuandika:" Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anategea pakubwa na hana turufu. Kilichoko matatani sio pekee masilahi ya wafanyakazi wa Uingereza bali pia yale ya wafanyakazi wa Ujerumani. Ripoti iliyochapishwa mwishoni mwa wiki na mtaalam kutoka Halle, imeweka wazi kabisa. Na ndio maana wakati umewadia kwa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya kutosubiri tena na badala yake kubuni mpango mbadala ili kuyanusuru japo nusu njia makubaliano ya Brexit."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ILnandspresse

Mhariri: Josephat Charo