1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika wamalizika mjini Lisbon

Josephat Charo10 Desemba 2007

Katika mkutano huo mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya umoja pande hizo mbili, EPA, ilitarajiwa kusainiwa lakini hakukupatikana makubaliano.

https://p.dw.com/p/CZdB
Rais wa Senegal Abdoulaye Wade akiuhutubia mkutano wa LisbonPicha: AP

Mkutano ya mjini Lisbon jana ulifikia makubaliano fulani kuhusu mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika.

Rais wa Senegal Abdoulaye Wade alilazimika kuondoka kutoka ukumbi wa mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na bara la Afrika mwendo wa tano asubuhi jana, saa moja kabla mkutano kumalizuka rasmi, kwa sababu alikuwa na shughuli nyingine muhimu nchini Senegal.

Wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari rais Wade alisema anaungana na viongozi wengine wa Afrika kupinga mikataba ya EPA.

´Kwangu mimi binafsi imedhihirika wazi kwamba bara la Afrika haliitaki mikataba ya EPA. Hilo nimelielewa kama jambo la msingi. Mambo mengine yaliyojadiliwa kwa mfano mswala ya afya, vijana na mengineyo, yote ni mazuri. Lakini mikataba ya EPA naipinga pamoja na viongozi wenzangu wa nchi za Afrika. Hatuitaki mikataba hii. Sasa tutakutana ili tujadiliane tunachokitaka badala ya mikataba hii ya EPA.´

Tangu mwaka wa 2002 Umoja wa Ulaya umekuwa ukifanya mazungumzo na nchi za Afrika kuhusu mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi. Mikataba hiyo inatakiwa isainiwe kufikia mwishoni mwa mwaka huu kwa kuwa kipindi cha mpito cha shirika la biashara la kimatiafa, WTO, kitamalizika wakati huo.

Katika mikataba hiyo nchi za Afrika, Karibik na Pacifik zinataka bidhaa zao ziruhusiwe kuingia masoko ya Ulaya bila kutozwa kodi. Nchi hizo zinakabiliwa na shinikizo la kusaini mikataba hiyo huku zikihofu kampuni zao hazitaweza kushindana na kampuni za Ulaya iwapo zitalazimika kuyafungua masoko yao.

Umoja wa Ulaya unasema utasaidia kifedha biashara ili waafrika waweze kununua bidhaa kwa bei nafuu. Hata hivyo unataka kampuni zake ziruhusiwe kuuza bidhaa zao barani Afrika.

Kwenye mkutano wa Lisbon nchi nyingi za kiafrika hazikufuahishwa na mikataba ya EPA. Hata hivyo waziri wa maendeleo wa Ureno, Joao Gomes Cravinho alisema mikata hiyo inatakiwa isainiwe kufikia mwisho wla mwaka huu.

´Karibu nchi zote, ikiwa sio zote, zitakuwa zimesaini mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.´

Kingozi wa halmashauri ya Umoja wa Ulya, Jose Manuele Barroso, amesema hawalazimishi mikataba ya EPA isainiwe kwa haraka.

´Hatushinikizi kwa njia yoyote mikataba ya EPA isainiwe haraka. Tunataka kuwepo makubaliano ili biashara isitatizike kuanzia Januari mosi mwakani. Tuna muda wa kutosha kuweza kufanya majadiliano mazuri na kuwa na maelewano mazuri katika maswala ya maendeleo na biashara.´

Lakini kufikia jana katika tovuti ya halmashauri ya Umoja wa Ulaya bado kulikuwa na ujumbe kwamba mikataba hiyo inatakiwa isainiwe kabla Januari mosi. Lakini kwa mujibu wa matamshi ya Jose Manuel Barroso hilo halitawezekana.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema ipo haja ya kufikia makubaliano ya muda kwa kuwa hakujafikiwa makubaliano kuhusu mikataba ya EPA.

´Naamini sote tungependelea tuyafikie makubaliano. Je itakuwaje ikiwa makubaliano hayo hayatafikiwa? Ikiwa hakutakuwa na makubaliano nchi kadhaa hasa nchi zinazoendelea za kiafrika zitaendelea kuwa na uhusiano mbaya wa kiabishara kati yao na umoja na Ulaya. Hilo hatulitaki. Nchi zilizo maskini zaidi hazitaathirika lakini zile ambazo tayari zimepiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi ndizo zitakazoathirika sana. Hilo nalo hatulitaki na wala nchi hizo pia hazilitaki. Ndio maana nasema tuwe wakakamavu, tuendelee kujadiliana. Tunataka tufikie makubaliano.´

Mkutano wa Lisbon nchini Ureno umedhihirisha kwamba mazungumzo kuhusu mikataba ya EPA yanatarajiwa kuendelea kwa muda usiojulikana na hakuna dalili ya makubaliano hayo kufikiwa hivi karibuni.