1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano ujao kati ya Israel na Palestina

11 Oktoba 2007

Barua ya watungaji 8 wa zamani wa sera za Marekani imetoa mashauri kadhaa ya kuweza kufikiwa suluhisho baina ya waarabu na waisrael.

https://p.dw.com/p/C7i2

Mwezi ujao utapofanyika mkutano maalumu kati ya wapalestina na Waisraeli, unabidi kuweka msingi wa sura ya amani ya kudumu itakavyokua pamoja na kuzishirikisha nchi za kiarabu ambazo sasa haziitambui Israel mfano wa Syria-hii ni kwa muujibu wa barua aliopelekewa juzi rais George Bush wa Marekani na kikundi cha watungaji wa 8 wa sera za Marekani.

Mkutano huo utumiwe pia kuanzisha jukwaa la mazungumzo ya amani kati ya Israel na Syria na uweke msingi wa kusimamishwa mapigano kati ya Israel na mwambao wa Gaza- ikiwa hatua ya kwanza kuelekea kukishirikisha chama cha Hamas kinachoudhibiti mwambao wa Gaza katika juhudi za amani-barua ilisema.

Barua hiyo imetiwa saini na washauri wa usalama wa Taifa wa zamani Zbgigniew Brzezinski na Brent Scowcroft miongoni mwa wengine.

Ili kuonesha uaminifu kwa nchi za kiarabu zinazoshiriki mazungumzoni,mkutano uliopangwa Novemba 15 huko Annapolis,Maryland,Israel inapaswa ichukue binafsi hatua ya kusimamisha utanuzi zaidi wa maskani za wayahudi-ilitaja barua ambayo ilitiwa pia saini na mrepublican wa zamani Lee Hamilton –mwenyekiti wa pamoja wa lile kundi juu ya Iraq pamoja na waziri wa nje wa zamani James Baker.

“ni vigumu kufanya mazungumzo yenye maana ya amani wakati ujenzi wa maskani unaendelea”-barua iliongeza.

Ikasema kwamba juhudi pia zichukuliwe kurahisisha hali za maisha za wakaazi katika gaza na kuruhusu kuanza upya kwa shughuli za biashara.

Mwambao wa Gaza unaodhibitiwa na chama Cha Hamas tangu majeshi yake kuyatimua yale ya chama cha FATAH cha rais Mahmoud Abbas Juni mwaka jana, umewekewa vikwazo vikali vya kiuchumi na Israel ili kuulemaza.Ni vikwazo vilivyoruhusu tu shehena za kibinadamu kuwafikia wakaazi wake milöioni 1.3.

Barua hii imeibuka wakati pakiwapo mabishano makali baina ya rais Mahmoud Abbas wa Palestina na waziri mkuu Ehud Olmert wa Israel yanayotangulia kikao hicho cha mwezi ujao.Pia yanafuatia kuchapishwa mwezi uliopita kwa barua nyengine kutoka mabalozi 5 wa zamani wa Marekani waliotumika muda mrefu nchi za mashariki ya kati.

Barua hii imemtaka waziri wa nje Dr.C.Rice kuimarisha juhudi zake binafsi ili kuhakikisha mazungumzo yajayo yanahetimishwa kwa ufanisi.

Barua halkadhalika, inaitaka Marekani kutoa mapendekezo yake ya kuziba mwanya wowote na kumtumia sana mjumbe wa kundi la pande 4-Quartet” –wauziri-mkuu wa zamani wa uingereza Tony Blair. Shabaha ni kupunguza tofauti baina ya pande hizo mbili kabla mkutano wa Maryland kufanyika.

Barua imeitaka pia Marekani ichukue hatua kuwaingiza Hamas na Syria,katika harakati hizi ili wasije wakaharibu mazungumzo.

Barua zote mbili zilizotoka zimesisitiza kwamba taarifa yoyote ya mwisho itakayotolewa juu ya mazungumzo hayo ya Novemba yaingize maelewano yalioafikiwa na pande mbili Israel na Palestina kuhusu mada 5 muhimu ambazo ni shina kwa suluhisho lolote litakalofikiwa.Maelewano hayo baadae yajumuishwe katika azimio la baraza la Usalama la UM.

Mada hizo 5 ni pamoja na kuundwa kwa dola la wapalestina katika mipaka ya 1967,kutambuliwa kwa Jeruselem kama mji mkuu wa dola zote mbili-Israel na Palestina huku mitaa ya wayahudi ikiwekwa chini ya mamlaka ya Israel na ile ya waarabu chini ya mamlaka ya wapalestina.Pia matayarisho maalumu yaafikiwe juu ya mji mkongwe wa Jeruselem yakihakikisha uhuru wa kila jamii kwenda katika vituo vyake vitakatifu.

Barua zote mbili halkadhalika, zinapendekeza maafikiano juu hatima ya wakimbizi wa kipalestina pamoja na kuwalipa fidia na misaada ya kujenga maskani mapya kwa wale wasiotaka kurudi kuishi katika dola jipya la wapalestina.