Mkutano wa AU waanza
15 Julai 2012Nkosazana Dlamini-Zuma kutoka Afrika kusini atapambana na rais wa sasa wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika , Jean Ping, baada ya wawili hao kushindwa kupata theluthi mbili ya kura zinazotakiwa katika mkutano uliopita , na kumuacha Ping katika wadhifa huo kwa miezi sita mingine. Watapambana tena leo wakiwania wadhifa huo, ambao Ping ameushikilia tangu mwaka 2008.
Wagombea wote wametoa taarifa kali kabla ya uchaguzi huo wa Jumapili. Mapema wiki hii , Ping alikanusha ripoti zilizotolewa na vyombo vya habari vya Afrika kusini kuwa atajitoa katika kinyang'anyiro hicho kumruhusu Dlamini -Zuma kugombea bila kupingwa, na kusababisha jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC kumshutumu Ping kwa kutumia vibaya mali za Umoja wa Afrika katika hatua za kuelekea katika uchaguzi huo.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema utamaduni uliopo ni kwamba mataifa makubwa katika bara hilo hayajiingizi katika kuwania wadhifa wa rais wa halmashauri ya umoja huo, na kuyaachia mataifa madogo kuchukua wadhifa huo, na uamuzi wa Afrika kusini kukiuka sheria hiyo ambayo si rasmi imezusha hisia mbaya.
Ping huenda akabakia rais
Iwapo itashindikana kumshagua rais wa halmashauri hiyo mara hii, Ping anaweza kisheria kubaki madarakani kama kiongozi hadi mkutano ujao Januari 2013.
Masuala ya kiusalama pia yanapewa umbele katika mkutano huo, huku viongozi wakiangalia zaidi kuhusu hali isiyo thabiti nchini Mali, ghasia zilizozuka tena katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na mzozo unaoendelea kati ya Sudan na Sudan kusini.
Kufuatia mkutano wa baraza la usalama na amani la umoja huo Jumamosi, umoja wa Afrika umetaka kukomeshwa kwa kile ulichokiita , uingiliaji kati usiokubalika, unaofanywa na uongozi wa zamani wa kijeshi nchini Mali kufuatia mapinduzi hapo Machi mwaka huu na kutoa wito wa kuvunjwa kwa utawala huo wa zamani wa kijeshi.
Congo na Rwanda kujadiliwa
Tawi la usalama la umoja huo wa Afrika pia limeitisha mkutano wa ngazi ya viongozi wa nchi kwa mataifa ya kieneo kutafuta suluhisho la ghasia zinazoongezeka mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.
Baraza hilo la usalama limehimiza kupatikana kwa suluhisho la haraka katika mizozo iliyopo kati ya Sudan na Sudan kusini mwishoni mwa mkutano wa usalama , ambao ulihudhuriwa na rais wa Sudan Omar al-Bashir na mwenzake wa Sudan kusini Salva Kiir.
Viongozi hao wa Sudan na Sudan kusini ambao nchi zao zilikaribia kupigana vita , walikutana Jumamosi kwa mara ya kwanza kwa mazungumzo ya faragha tangu kuzuka kwa mapigano.
Mkutano huo wa umoja wa Afrika unakwenda kwa kauli mbiu ya kuimarisha biashara baina ya mataifa ya Afrika, kama ilivyokuwa katika mkutano wa Januari wa umoja huo. Maafisa wanasema wameamua kuweka mada moja kila mwaka badala ya mada mpya katika kila kikao, kama ilivyokuwa hapo zamani.
Mkutano huo unafanyika katika mji mkuu wa Ethiopia , Addis Ababa baada ya rais mpya wa Malawi Joyce Banda kukataa kumwalika Bashir, ambaye anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na madai ya mauaji ya kimbari.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Idd Ismail Ssesanga