1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa biashara wa kimataifa kumalizika leo mjini Mombasa.

Saumu Mwasimba4 Machi 2005

Majadiliano yakusudia kufungua nafasi ya kupatikana mkataba wa biashara duniani fikapo 2006.

https://p.dw.com/p/CHhI
Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Peter Mandelson.
Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya Peter Mandelson.Picha: AP

Mazungumzo kwa ajili ya kuimarisha nafasi za kukamilishwa kwa mkataba wa biashara wa kimataifa ifikapo 2006, yaliligeukia suala tete la kilimo hii leo, huku kukiwa na majadiliano makali juu ya uamuzi muhimu wa Shirika la biashara dunia kuitaka Marekani aiache mtido wa kutoa ruzuku kwa wakulima wake wa pamba.

Wakati uamuzi wa jana wa Shirika la biashara duniani WTO ukiependelea Brazil na kuzusha sura ya hata mgawanyiko mkubwa zaidi kati ya kaskazini na kusini kuhusiana na ruzuku kwa wakulima, mawaziri wa biashara kutoka mataifa 33 walikutana kwa siku ya pili na ya mwisho hii leo.

Athari ya uamuzi huo ambao Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Brazil Celso Amorim aliutaja ni ushindi kwa nchi zinazoendelea, na ambao unailazimisha Marekani kuachana na mpango wake wa kuwalipa fidia ya mamilioni ya dola wakulima wake wa pamba, ni jambo lililojitokeza wazi mkutanoni.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Brazil alisema uamuzi huo unaweka bayana kwamba mtindo huo si halali.

Hata hivyo Mkuu wa masuala ya biashara wa umoja wa ulaya Peter Mandelson, alionekana kutounga mkono wazo la kwamba uamuzi huo utakua na athari kwa mazungumzo mapana zaidi.

Lakini akizungumza mjini washington, msemaji wa ofisi ya muakilishi wa biashara wa Marekani, alisema Marekani inauzingatia uamuzi huo wa WTO, ulioyapa haki malalamiko yaliowasilishwa na Brazil, kwamba mtindo wa utoaji ruzuku wa Marekani kwa wakulima wake unahujumu mashindano ya kibiashara kwa wakulima wa zao hilo duniani na kusababisha kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia.

Mbali na Brazil uamuzi huo umepongezwa pia na nchi zinazolima pamba katika eneo la Afrika magharibi na hasa Benin, Chad, Mali na Senegal ambazo kwa pamoja zimeitaka Marekani kuuheshimu na kuutekeleza haraka .Lakini bado haijafahamika wazi kama Marekani inakubaliana na uamuzi huo.

Wakati huo huo ulimwengu ulioendelea unashikilia kwamba mataifa masikini hayana budi kupunguza vikwazo vya forodha na vyenginevyo katika sekta ya biashara ili kufungua masoko yao kwa washindani kutoka nje, na hasa kwa bidhaa zisizokua za kilimo na katika sekta nyengine.

Kamishna wa biashara wa umoja wa Ulaya Bw Mandelson alisema ni jambo la kuvutia pamoja na hayo kuona kuna hatua ya maendeleo na kuongeza kwamba nchi kadhaa zikiwemo Brazil, Bangladesh, India ;Japan na Senegal zimetoa mchango kabambe katika taarifa na huduma zao, na kwamba zimetoa pia sura juu ya umuhimu,hali halisi na haja ya kujitolea ili lengo la kufikia mkataba wa kibiashara duniani liweze kutimizwa kama ilivyokusudiwa hadi ifikapo 2006.

Kwa upande mwengine Wakenya 43-waandamanaji walio wapinzani wa sera ya utanda wazi ambao walitiwa nguvuni jana walipojaribu kuelekea kwenye eneo la mkutano huo wa Mombasa walifikishwa katika mahakama ya mji wa Kwale kusini mwa Mombasa leo wakishitakiwa kwa makosa ya uhalifu ambapo hukumu dhidi yao inaweza kufikia kifungo cha miaka mitatu jela. Watatu miongoni mwao waliachiliwa huru baada ya kuungama makosa yao wakisema yametokana na hali ngumu ya maisha, na 40 wengine wakaachiwa kwa dhamana ya shilingi 10,000 za Kenya kila mmoja, hadi kesi itakaposikilizwa tena tarehe 18 ya mwezi huu . Mkutano huo wa mawaziri na maafisa wa biashara wa mataifa 33 unamalizika hii leo.