1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa dharura wa OIC mjini Istanbul,Uturuki

17 Agosti 2011

Jumuiya ya Mataifa ya Kiislam leo yaanza mkutano wake wa dharura huko Istanbul Uturuki kujadiliana jinsi ya kusaidia kukabiliana na hali mbaya ya ukame na njaa katika pembe ya Afrika.

https://p.dw.com/p/12ITG
Uturuki kunakofanyika mkutano wa OIC.Picha: DW

Somalia, Kenya na Ethiopia ni kati ya mataifa yaliyoathiriwa vibaya na hali hiyo ya ukame.

Nchi wananchama 57 za jumuiya hiyo zinakutana kufuatia ombi la Uturuki ambayo ndiyo mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa sasa, ili kujadiliana jinsi ya kuimarisha misaada kwa wahanga wa baa la njaa katika eneo hilo.

Mkutano huo unafanyika huku Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akitarajiwa kuondoka kesho kwenda Mogadishu Somalia akiandamana na Waziri wa Mambo ya Nje Ahmed Davutoglu pamoja na familia zao.

Wie US-Diplomaten Politiker einschätzen Flash-Galerie
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: AP

Viongozi hao watakwenda kuangalia jinsi usambazaji wa misaada ya Uturuki nchini Somalia unavyokwenda.Tayari Uturuki imekwishatuma ndege tatu zenye shehena ya misaada ya chakula na madawa kwa wasomali wakati wa mwezi huu mtukukufu wa Ramadhani.

Viongozi wa serikali za dunia kutembelea Mogadishu ni nadra sana kutokana na usalama hafifu.Lakini Waziri huyo mkuu wa Uturuki ambaye amekuwa shujaa miongoni mwa viongozi wa kiislamu kwa msimamo wake dhidi ya Israel, amesema ni vigumu kwao kubakia wakitazama tu jinsi maisha ya binaadamu yanavyohatarishwa barani Afrika.

Flash-Galerie Hungersnot Somalia
Hali mbaya ya njaa nchini SomaliaPicha: dapd

Kiongozi wa mwisho kuutembelea mji huo mkuu wa Somalia Mogadishu, ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda Novemba mwaka jana.

Naye Abdifatah Abdi Noor ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia amesema ziara hiyo ya Bwana Erdogan nchini Somalia ni nafasi muhimu sana kwani itazidi kuitanabahisha dunia juu ya hali nchini Somalia.

Televisheni za Uturuki zimekuwa zikionyesha picha za wahanga na hali mbaya ya njaa katika pembe ya Afrika, ikiwa ni katika harakati za kuhamasisha misaada kwa wahanga hao.

Katika kampeni za kukusanya fedha, zaidi ya Euro millioni 80 zimekwisha kusanywa, kampeni mbalimbali zikiwemo matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya mbio za Marathon zikiongozwa na wanasiasa mashuhuri halikadhalia wacheza sinema maarufu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kiasi cha watu milioni 12 wako katika hatari ya kufa kwa njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika, huku Somalia ikiwa imeathirika zaidi.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/APF/Reuters

Mhariri:Josephat Charo