Mkutano wa G20 waanza chini ya kiwingu cha janga la COVID-19
21 Novemba 2020Shughuli za mkutano huo wa kilele ambao kwa kawaida huwakutanisha ana kwa ana viongozi wa madola yenye nguvu zimepunguzwa na badala yake kutakuwa na majadiliano mafupi kupitia njia ya video kuhusu masuala tete yanayoukabili ulimwengu hususan athari za janga la virusi vya corona.
Kadhalika kutakuwa na mjadala kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa duniani
Saudi Arabia ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano huo wa siku mbili imekuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuandaa mkutano wa G20.
Rais Donald Trump wa Marekani atakuwa sehemu ya viongozi watakoshiriki mkutano huo wa kilele wa kundi la G20.
Taarifa hizo zimethibitishwa na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani ambaye amesema Trump atakuwa sehemu ya viongozi wa ulimwengu watakaoshiriki mkutano huo unaofanyika kwa njia ya video kutokana na janga la virusi vya corona.
G20 kutoa ahadi ya kumaliza kadhia ya corona
Kulingana na rasimu ya taarifa ya pamoja itakayotolewa na viongozi watakaohudhuria, kundi la G20 litaahidi kufanya kila linalowezekana kudhibiti kusambaa janga la virusi vya corona huku likitahadharisha kuwa ufufuaji wa uchumi wa dunia bado unakabiliwa na ukosefu wa usawa na mazingira yasiyotabirika.
Viongozi wa kundi hilo wametanabaisha kuwa mzozo wa virusi vya corona umeziathiri zaidi jamii masikini na kusema mataifa yanayoendelea yatahitaji msaada zaidi wa kupunguziwa mzigo wa madeni hata baada ya kipindi cha sasa cha hadi mwishoni mwa mwezi Juni, 2021.
Kabla ya kuanza mkutano wa leo, shinikizo limetolewa la kutaka kundi la mataifa ya G20 kufidia nakisi ya dola bilioni 4.5 iliyopo kwenye mpango wa kusambaza chanjo ya virusi vya corona wa shirika la afya duniani WHO na kufungua njia ya kumalizika kwa janga hilo.
Barua iliyotumwa kwa G20 na kutiwa saini na viongozi wa Norway, Afrika Kusini, mkuu wa WHO pamoja na rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inawarai viongozi wa kundi hilo kutoa ahadi ya kuwekeza kiwango hicho cha fedha ili kuokoa maisha kwa kusaidia ununuaji na usambazaji wa shehena kuwa ya dozi za chanjo ya virusi vya corona kote ulimwenguni.
Wito kama huo umetolewa pia na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyewataka viongozi wa mataifa hayo yenye nguvu kuongeza mshikamano katika wakati anapigania usambazaji wa usawa kwa chanjo ya virusi vya corona.
Guterres amesema anatumai mpango wa usambazaji chanjo chini ya Umoja wa Mataifa utakuwa njia madhubuti ya kuhakikisha kuwa chanjo ya COVID-19 itakuwa bidhaa ya walimwengu wote na itapatikana kwa wakati na kwa njia nafuu na kuyataka mataifa ya G20 kuunga mkono mradi huo unaofahamika kama Covax.