Mkutano wa Hamas na Mahmud Abbas utazaa matunda?
20 Julai 2012Hayo yanatukia huku kukiwa na ufuatiliaji wa jinsi gani sera ya Misri kwa Wapalestina itakavyobadilika.
Katika mazungumzo yao, Mursi alihakikisha kuwa atawasaidia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ambao unatawaliwa na Chama cha Hamas, kwa mujibu wa maelezi ya Meshaal.
Kauli hiyo, amesema kiongozi huyo wa Hamas, kuwa inatoa matumaini ya mwanzo mpya wa uhusiano baina ya Misri na Palestina.
Shirika la Habari la Taifa la Misri, Mena, limeandika juu ya habari hii, huku likimnukuu Meshaal akipongeza kufanyika kwa mkutano huo ambao ameuita ni wa kihistoria. Itambulike kuwa mkutano huo ni wa kwanza kati ya ujumbe wa chama hicho cha Kipalestina na kiongozi wa Misri.
Maudhui hasa ya mkutano huo ni yepi?
Adha, viongozi hao wawili walijadiliana juu ya namna ya kuhakikisha Gaza inapata nishati ya gesi na petroli ambayo inahitaji licha ya Israeli kuufunga mpaka wakeKikao hicho kilidumu kwa zaidi ya saa mbili, tofauti ya saa moja aliyoitumia Mursi alipokutana na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Palestina na kiongozi wa kundi la Fatah.
Kwa sehemu, Israeli na Misri zimeufunga Ukanda wa Gaza, ambao uko jirani na nchi hizo mbili, tangu mwaka 2007 baada ya Hamas kukitimua kwa nguvu chama cha Abbas, kutoka ukanda huo.
Rais aliyengólewa madarakani, Hosni Mubarak, aliregeza uzio na vikwazo ilivowekewa Gaza mwaka juzi, lakini hakuruhusu bidhaa za biashara kupitishiwa katika mpaka wa Rafah, kama Hamas walivyotarajia.
Chini ya utawala wa Mubarak, Misri ilijaribu kuleta mapatano baina ya Fatah na Hamas, ambayo yaliasisiwa wakati kila upande ukiushutumu mwingine.
Meshaal amesema Mursi yuko mbioni kukutana nae pamoja na Abbas kujadili kwa pamoja kuweka msukumo wa kufikiwa kwa umoja thabiti.
Hamas na Fatah waliingia makubaliano mwaka 2010
Chama cha Fatah ambacho kinatawala katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Hamas, wanaotawala Ukanda wa Gaza, waliingia makubaliano ya kitaifa mwezi Aprili mwaka jana, mjini Cairo, kwa jitihada za Misri.
Katika makubaliano hayo, serikali hizo mbili zinapaswa kumteua kiongozi asiyeegemea upande wowote ule, na kupewa jukumu la kuandaa zoezi la uchaguzi katika kipindi cha miezi 12. Hatahivyo, mkataba huo bado umebaki kwenye karatasi tu.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul
Mhariri: Miraji Othman