Mkutano wa Helsinki na Kombe la dunia 2018 Magazetini
16 Julai 2018
Tunaanzia Helsinki, Finnland, ambako rais wa Marekani Donald Trump atakutana na kiongozi mwenzake wa Urusi Vladimir Putin. Kawaida mikutano ya kilele kama huu inapoitishwa Helsinki, walimwengu hutarajia faraja katika uhusiano kati ya madola makuu. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linaandika: "Makubaliano kati ya Putin na Trump yanawezekana pia. Watakaokumbwa na mashaka hapo ni mataifa ya Umoja wa Ulaya ambayo Trump ametishia mjini Brussels kuyapa kisogo. Na hilo ni lengo ambalo Putin, sawa na viongozi wa zamani wa Usovieti na Urusi amekuwa akilifuata. Msimamo wa pamoja unakutikana pia katika azma ya kuugawa Umoja wa Ulaya. Moscow inalifuata lengo hilo kwa nguvu kwa kuunga mkono makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia."
Chuki za Trump dhidi ya Umoja wa Ulaya
Trump pia hafichi msimamo wake dhidi ya Umoja wa Ulaya. Anafika hadi ya kumshauri waziri mkuu wa Uingereza Theresa May atangulize mbele malumbano badala ya majadiliano katika mipango ya kuitoa nchi yake katika Umoja wa ulaya. Gazeti la "Straubiger Tagblatt/Landshuter Zeitung" linaandika: "Tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita, Theresa May amepokea mashauri ya kila aina-mema na yanayoashiria mema kuhusiana na suala vipi matakwa ya idadi kubwa ya waingereza, ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, yatakavyoweza kutekelezwa. Hakuna shauri hata moja lilililoonyesha kuwa la upuuzi kama hili alilopewa na rais wa Marekani Donald Trump: badala ya kuendeleza mazungumzo ya muda mrefu, bora waziri mkuu aufikishe mahakamani Umoja wa Ulaya. Shauri hilo linadhihirisha chuki aliyonayo Donald Trump na mashabiki wake wa Uingereza dhidi ya taasisi hiyo ya mjini Bruissels."
Subira yavuta kheri
Na hatimaye wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamechambua kwa mapana na marefu ushindi wa timu ya taifa ya Ufaransa-"Les Bleus"katika fainali ya kombe la dunia la kabumbu dhidi ya Croatia."Gazeti la "Weser Kurier" linaandika" "Kocha Didier Deschamps amefanikiwa kufanya kile ambacho Joachim Löw kimemshinda msimu huu wa kiangazi:Kuteremsha timu ya wenye kujipendelea na kujipigania uwanjani, timu iliyoungana kwa lengo moja tu, nalo ni kurejea nyumbani na Kombe la dunia. Ufaransa ilibidi isubiri Miaka 20 kuweza kuvikwa kwa mara ya pili taji la mabingwa wa dunia. Na kila mwenye kufuatilizia hali namna ilivyo katika shirikisho la kabumbu nchini Ujerumani-DFB basi hatokosa kugundua muda kama huo huenda ukahitajika kwa timu ya taifa ya Ujerumani pia."
Lilian:
Na kwa hayo ndio na sisi tunazifunga kurasa za magazeti ya Ujerumani toka DW Bonn..................................
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Josephat Charo