Mkutano wa Kampala na majaaliwa ya Kongo
7 Agosti 2012Lakini maslahi ya mataifa hayo yanayokinzana yanaweka juhudi hizo mashakani. Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda umeshuka kwa kiwango kikubwa katika siku za hivi karibuni. Hata hivyo, suluhisho la kisiasa na kijeshi la mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo haliwezi kupatikana bila kuzishirikisha nchi hizi mbili. Kwa kujua hili, wakuu wa nchi za maziwa makuu wanakutana Jumanne mjini Kampala kujadili kuundwa kwa kikosi cha pamoja kukabiliana na waasi.
Katikati ya mwezi wa Julai mkutano mkuu wa mataifa yanayounda kanda ya maziwa makuu (ICGLR) ambayo ni jirani na Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yalikubaliana mjini Addis Ababa kuunda kikosi kisichoegemea upande wowote, ikiwezekana kwa kusaidiwa na Umoja wa Afrika au Umoja wa Mataifa. Mpango huu ndiyo unatakiwa kukamilishwa na mkutano wa Kampala.
Maslahi kinzani ni kikwazo kwa suluhu ya kudumu
Lakini Ilona Auer-Frege kutoka mtandao wa Ekumeni wa Afrika ya Kati anaona kuwa maslahi yanayokinzana katika mgogoro huu yanaweza kuwa kizingiti kikubwa katika upatikanaji wa suluhu. "Ugumu wa ICGLR ni kwamba wanachama wana maslahi tofauti na hii inaweza kuwa vigumu sana kwao kukaa meza moja na hii inaoneka sasa katika mgogoro huu. Wako katika shinikizo kutoka wafadhili wa kimataifa kukubaliana, lakini kwa upande mwingine, kila moja ana maslahi tofauti na hii ni ngumu kweli," anasema.
Lengo la operesheni hiyo ni kukabiliana na waasi wa M23 wanaoongozwa na Sultan Makenga na Bosco Ntaganda na ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya mkoa wa Kivu Kaskazini na sasa wanatishia kuukamata mji muhimu wa Goma. Lakini maslahi ni tofauti. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaishtumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi, madai ambayo yalithibitishwa na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyochapishwa mwezi Juni. Kwa upande wake, Rwanda inakusha madai hayo na pia inapingana na ushahidi uliotolewa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Utetezi wa Rwanda
Rwanda inaweza kudai kuwa kikosi hicho kisitumike tu dhidi ya waasi wa M23, bali pia dhidi ya makundi yote ya waasi yaliyoko mashariki mwa Kongo, na hiyo itamaanisha hata waasi waliosalia wa kundi la Demokratic Forces for the Liberation of Rwanda, FDLR, linaloundwa na Wahutu ambao wanatuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Na hapo lengo linalokusudiwa la kupambana na waasi wa M23 litakuwa limepunguzwa nguvu, anasema Ilona Auer Frege. Lakini waziri wa mawasiliano wa Kongo Lambert Mende bado anauona mkutano huu kama hatua muhimu.
"Kwa bahati mbaya majirani zetu wanaamini kuwa laazima upambane na waasi wa FDLR na M23 wasiguswe na tunashangaa kwa nini hii inakuwa hivyo. Watu wanauawa na makundi haya mawili na laazima yote yakomeshwe. Lakini kuna mafanikio yaliyopatikana mjini Adis Ababa ambapo rais Kagame alisaini waraka unayoyataja makundi haya yote kama yanayopaswa kupingwa. Hivyo kuna mwanga."
Kutokubalika kwa rais Kabila Mashariki mwa Kongo
Katika mazungumzo hayo, Rwanda inatumia fursa ya kutokubalika sana kwa Rais Joseph Kabila mashariki mwa Kongo. Jaribio la Rais Kabila kutaka kumkata Bosco Ntaganda na kumfikisha katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu limekuwa na madhara makubwa kwake. Ntaganda ambaye aliingizwa katika jeshi la Kongo kama sehemu ya mpango wa amani mwaka 2009, alilitoroka jeshi hilo na kuanzisha kundi la M23 ambalo liliweza kuchukua maeneo kadhaa katika muda mfupi pasipo na upinzani mkali kutoka vikosi vya serikali.
Lakini Rwanda inaonekana kubanwa kila kona kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa ambapo wafadhili wake wakuu, nchi za Marekani, Ufaransa, Uholanzi na Ujerumani ziliamua kusitisha msaada kwa nchi hiyo. Hali hii, anasema Auer-Frege, haitoiacha Rwanda bila madhara:
"Katika mazungumzo hayo laazima Rwanda ionyeshe kuwa iko tayari kushiriki kikamilifu katika kutatua mgogoro huu, na kwamba nchi hiyo haiwezi kuendelea kutumia ubabe kama ilivyo kuwa inafanya," anafafanua.
Miongo karibu miwili ya mgogoro wa Kongo imekuwa ikiamuliwa kwa maslahi ya mataifa tofauti ya kanda ya maziwa makuu. Rais Laurant Kabila alifanikiwa kumaliza utawala wa miaka 30 ya rais Mobutu Tseseko kwa msaada wa nchi jirani zikiwemo Rwanda, Uganda na Angola na kisha kujitangaza yeye kama rais.
Matumaini finyu ya ufanisi
Chini ya mwaka moja baadaye washirika hawa walikuwa wamegawanyika, na Kongo pia. Wakati mazungumzo ya amani yalilenga kuinganisha Kongo, bado wengi wananufaika na kukosekana kwa usalama na miundombinu dhaifu nchini humo. Uganda pia ina maslahi ya kiuchumi nchini Kongo, anasema Auer-Frege.
"Kwa hiyo nadhani wakati mwingine kuna haja ya kutathmini maslahi ya nchi katika Kongo. Kwa maslahi yake, ushiriki wa Uganda katika mgogoro wa kongo siyo mkubwa kama ilivyo kwa Rwanda. Vingenvyo nadhani mataifa mengine yatajiweka mbali na mgogoro huo au yatalaazimika kuingia katika mgogoro huo kuliko wasivyotaka. Wao wana maslahi zaidi katika utulivu."
Pia, maslahi sawa ya kundi la ICGLR ambalo liliundwa kama shirikisho la mataifa kwa shinikizo la Umoja wa Mataifa ni madogo sana. Wachambuzi wengi wanaona matumaini madogo ya ufanisi wa Mkutano huu kutokana na hali mbaya ya kifedha kwa kuwa hata kile kikosi cha Umoja wa Afrika kilichoundwa mwaka 2005 kwa ajili ya Kongo bado kutimiza malengo yake.
Mwandishi: Sandler Philipp/ MMD Afrika
Mfasiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohammed Khelef