1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele kati ya Afrika na Marekani kuhusu biashara kuanza Jumatano mjini Cape Town

Josephat Charo13 Novemba 2007

Viongozi wa Marekani na Afrika watakutana mjini Cape Town nchini Afrika Kusini kuanzia kesho Jumatano kwenye mkutano wa kilele utakaojadili biashara na uwekezaji.

https://p.dw.com/p/CH6y

Zaidi wa wajumbe 1,000 wanatarajiwa kuhudhira mkutano wa kilele kuhusu biashara kati ya Marekani na bara la Afrika, ambao huandaliwa na baraza la mashirika ya kibiashara ya Afrika, CCA. Mkutano huo wa kilele ambao kitamaduni hufanyika mara mbili kila mwaka, ni wa sita.

Baraza la mashirika ya kibiashara ya Afrika lilianzishwa mnamo mwaka wa 1993 na hushirikiana na serikali, mashirika ya kimataifa na ya kibiashara kulitangaza bara la Afrika kama kituo muhimu cha uchumi na uwezekaji kwa makampuni ya Marekani.

Mkutano wa mjini Cape Town nchini Afrika Kusini, uliopewa jina, Africa: Entering the Door to opportunity, yaani jinsi Afrika inavyoweza kujikwamua na kutumia uwezo wake ili inufaike, ni wa kwanza wa aina hiyo kufanyika barani Afrika.

Bara la Afrika ambalo lilifurahia ukuaji wa kiuchumi kwa asilimia 5.5 mwaka jana, na kiwango cha chini zaidi cha kasi ya mfumuko wa bei katika kipindi cha miaka 30, linawavutia upya wawekezaji wa kigeni. Marekani ni nchi pekee iliyo mshirika mkubwa wa bara la Afrika huku biashara kati ya Marekani na bara hilo ikifikia dola bilioni 71 za kimarekani mnamo mwaka jana.

Bidhaa nyingi zinazonunuliwa na Marekani kutoka Afrika huingia nchini humo bila kutozwa kodi kulingana na mkataba wa AGOA uliosaniwa mnamo mwaka wa 2000. Lakini Marekani inakabiliwa na hatari ya kushindwa na China barani Afrika, ambayo biashara yake na bara hilo iliongezeka mara kumi kufikia dola bilioni 40 za kimarekani kati ya mwaka wa 1995 na 2005.

Kampuni za China zimekuwa pia zikiwekeza mabilioni ya dola katika uwekezeji wa kigeni usio na masharti katika migodi barani Afrika, miradi ya ujenzi wa miundombinu na mabenki. Juhudi za China barani Afrika zimezusha shutuma kwamba inaongoza juhudi za ukoloni mamboleo barani Afrika.

Wawekezaji wa Marekani wakilinganishwa na Wachina, wamekuwa waangalifu katika siku za hivi karibuni kuhusu maswala ya Afrika aidha kwa sababu ya uzoefu wa zamani au hatari ya kuwekeza barani humo. Hata hivyo nchi za Afrika zimejidhihirisha kuwa vivutio muhimu kwa wawekezaji, hivyo kuzipa fursa kampuni za Marekani katika sekta ya uchimbaji madini, utalii na ujenzi ya miundombinu.

Wajumbe wa kampuni kubwa za Marekani, zikiwemo Coca-Cola, General Motors na kampuni kubwa ya kuchimba madini ya almasi, De Beers, watajadili nafasi zilizopo za kibiashara kati ya Marekani na Afrika kwenye mkutano wa mjini Cape Town. Waliouandaa mkutano huo wanasema utasisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha maendeleo endelevu.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini anatarajiwa kuufungua mkutano huo hapo kesho. Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni na waziri wa fedha wa Marekani, Henry Paulson, ni miongoni mwa viongozi wa kisiasa wa ngazi ya juu wanaotarajiwa kuhutubia mkutano huo utakaomalizika Ijumaa wiki hii.

Uhusiano kati ya Afrika na Marekani umekabiliwa na matatizo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na juhudi za Marekani kutafuta makao ya kikosi chake cha jeshi AFRICOM, barani Afrika. Pendekezo hilo limepingwa na nchi kadhaa za kiafrika zenye ushawishi mkubwa zikiwemo Afrika Kusini na Libya. Liberia ni nchi pekee ambayo imeashiria kuwa tayari kuruhusu kambi ya kikosi cha Marekani barani Afrika ijengwe katika ardhi yake.