1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa APEC mjini Sydney

Oummilkheir7 Septemba 2007

Viongozi wa APEC wazozana bado katika suala la hali ya hewa

https://p.dw.com/p/CH8M
Maandamano ya Sydney dhidi ya sera za Marekani nchini Irak
Maandamano ya Sydney dhidi ya sera za Marekani nchini IrakPicha: AP

Wakuu wa nchi zinazopakana na bahari ya Pacific-APEC wanaokutana mjini Sydney nchini Australia,wanashindwa kuafikiana juu ya taarifa ya mwisho kuhusu hali ya hewa-kabla ya taarifa hiyo kuidhinishwa na viongozi wa jumuia hiyo mwishoni mwa wiki hii.

Baada ya mazungumzo kusita katika hali ya mvutano asubuhi ya leo,maafisa hao wa ngazi ya juu wamepangiwa kukutana tena baadae hii leo-hayo lakini ni kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja ambae hakutana jina lake litajwe.

“Bado hakuna maridhiano yaliyofikiwa kuhusu malengo halisi na ratiba ya kuyafikia malengo hayo” mwanadiplomasia huyo amesema.

Kwa mujibu wa maafisa wa ngazi ya juu na wataalam,Marekani na Australia wanajaribu kuzishawishi nchi nyengine,kati ya 21 za APEC zijiunge na duru mpya za mikutano kuhusu hali ya hewa-duru ambazo hazitolingana kabisa na itifaki ya Kyoto kuhusu kupunguzwa gesi za sumu zinazotoka viwandani.

Marekani na Australia ni nchi pekee zilizoendelea ambazo hazikuidhinisha itifaki ya Kyoto inayosimamiwa na Umoja wa mataifa na ambayo muda wake utamalizika mwaka 2012.

Mataifa kadhaa yanapendelea kuuona Umoja wa mataifa ukiendelea kuwa mhimili wa mazungumzo kuhusu hali ya hewa.

Rais George W. Bush wa Marekani,anaehudhuria mkutano huo wa kilele wa nchi zinazopakana na bahari ya Pacific-APEC aliteleza ulimi aliposema:

“”Ahsante waziri mkuu kwa maelezo yako.Ahsante kwa ukarimu wako katika mkutano huu wa kilele wa OPEC.Nimeridhishwa na mkutano wa kilele wa APEC.Amenialika katika mkutano wa kilele wa OPEC mwakani-Mkutano wa kilele wa APEC….”

Rais huyo wa Marekani aonyesha kuchanganya jumuia ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC na hii ya mataifa yanayopakana na bahari ya Pacific APEC ambayo viongozi wake wanakutana Sydney nchini Australia.

Mbali na suala la hali ya hewa,viongozi wa mataifa ya APEC wanatazamiwa kutia saini taarifa kuhusu usalama wa chakula na ubora wa bidhaa-katika wakati ambapo jamahuri ya umma wa China inajikuta ikitiwa kishindo ipitishe hatua zinazofaa kulinda afya ya wanunuzi.

Serikali ya mjini Beijing imekua ikilaumiwa na walimwengu mnamo siku za hivi karibuni kwa sababu ya kutengeneza bidhaa hatari kwa afya.

Rais Hu Jintao wa China ametetea hapo jana ubora wa mazao ya chakula yanayosafirishwa na nchi yake nchi za ng’ambo akisema asili mia 99 ya mazao hayo ni salama.

Mradi wa Marekani wa kutega mtambo wenye nguvu za kudengua makombora ya adui barani Ulaya ,uligubika mazungumzo kati ya rais George W. Bush na kiongozi mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mjini Sydney.

Baada ya mazungumzo yao pembezoni mwa mkutano wa kilele wa APEC,rais Putin aliwaambia waandishi habari wataalam wa nchi hizi mbili watakutana hivi karibuni na kuutembelea mambo wa Radar uliowekwa Azerbaidjan.Serikali ya Urusi imeishauri Marekani iutumie mtambo huo badala ya kuteka mitambo mengine katika jamhuri ya Tcheki na Poland.