1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa umoja wa ulaya na nchi sita za Mashariki mjini Prague

Oumilkher Hamidou7 Mei 2009

Viongozi wanapanga kutia saini mkataba wa Ushirikiano

https://p.dw.com/p/HlZx
Mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Javier SolanaPicha: AP


Mataifa ya Umoja wa Ulaya yanakutana na mataifa sita ya jamhuri za zamani za Usovieti kwa mazungumzo yaliyolengwa kuendeleza hali ya utulivu na kupunguza ushawishi wa Urusi bila ya kuiudhi serikali ya mjini Moscow au kuyapa moyo matumaini yao kuelekea Umoja wa Ulaya.

Lengo kuu la ushirikiano wa aina mpya pamoja na nchi za mashariki ni "kuharakisha ushirikiano wa kisiasa na mafungamano ya kiuchumi kati ya wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya na Armenia,Azerbaidjan,Byelorus,Georgia,Moldova na Ukraine"-hayo ni kwa mujibu wa mswaada wa taarifa ya mwisho inayotazamiwa kutiwa saini mwishoni mwa mkutano huo.

Matamshi kama hayo hayatarajiwi kupunguza makali ya upinzani wa Urusi kwa mpango huo ambao Moscow unauangalia kama njama ya kutaka kuidhoofishia ushawishi wake katika eneo hilo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi,Sergei Lavrov alionya jana dhidi ya "kuchorwa mistari mipya ya mgawanyiko" barani Ulaya.

Russland Außenminister Sergej Lawrow zu Georgien Abchasien und Südossetien
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi LavrovPicha: AP

Hata hivyo mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya,Javier Solana,amehakikisha mjini Prague akisema tunanukuu:"ushirikiano pamoja na nchi za Mashariki,haujalengwa dhidi ya Urusi ambayo pia tunashirikiana nayo."Mwisho wa kumnukuu muakilishi mkuu wa siasa ya nje wa umoja wa ulaya.

Halmsahrui kuu ya Umoja wa ulaya mjini Brussels inasema mkakati huu mpya umelengwa kuimarisha hali ya utulivu katika eneo hilo .

Vita na mivutano ya kisiasa nchini Georgia,machafuko nchini Moldova na misuko suko ya kisiasa na kiuchumi nchini Ukraine,yote hayo yanaashiria haja ya kuchukuliwa hatua,lakini baadhi ya mambo yamekiuka mipaka ya ushirikiano.

Mkakati huo umebuniwa na jamhuri ya Cheki ambayo ndio mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya hadi mwishoni mwa mwezi ujao.

Lakini serikali ya Cheki imeporomoka na serikali ya mpito inatazamiwa kuapishwa kesho.

Prague imeshindwa kuwashawishi viongozi wa Umoja wa ulaya -mfano wa waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown,rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy,waziri mkuu wa Hispania Jose Luis Rodriguez Zapatero na mwenzake wa Italy,Silvio Berlusconi wahudhurie mkutano huo utakaoanza leo jioni.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amesema kutokuwepo Sarkozy mkutanoni kunazidisha "hatari " ya siasa kuelekea Mashariki,iliyobuniwa na nchi zinazotokea Mashariki na siasa kuelekea nchi za Mediterenia iliyobuniwa na nchi zinazopakana na bahari ya Mediterenia."

Mswaada wa taarifa ya mwisho unabainisha kuna mvutano kuhusu namna ya kuzijongelea nchi za mashariki,na kwamba marekebisho ya taarifa hiyo yanafafanua msimamo wa nchi za magharibi-Ufaransa,Ujerumani na nchi za Benelux,yaani Ubeligiji,Uholanzi na Luxembourg ambazo zinapendelea watu wasende mbali sana.

Mataifa hayo sita yanatajwa wazi kabisa katika taarifa hiyo ya mwisho kama " Nchi shirika za Ulaya ya Mashariki".Kumewekwa masharti pia yanayozungumzia juu ya kutokuwepo ushirikiano wowote na nchi za mashariki bila ya kuwepo hatua za kweli kuelekea demokrasia na maendeleo ya kiuchumi katika nchi zote hizo sita.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman