Mkutano wa hatma ya misitu ya Kitropiki waendelea Kongo
27 Oktoba 2023Jumamosi, 27.10.2023, itakuwa zamu ya wakuu wa nchi kuhudhuria mkutano huo.
Waratibu wa mkutano huo wa kilele wanasema kuwa wakuu wa mataifa kadhaa ya Afrika yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Rwanda, Gabon, Togo, Guinea-Bissau na Comoro wanatarajiwa kuhudhuria sambamba na mwenyeji, Rais Denis Sassou Nguesso.
Hata hivyo hakuna mkuu wa nchi yoyote inayozungukwa na misitu ya Amazon au bara la Asia atakayekuwemo kwenye mkutano huo.
Waziri wa mazingira wa Kongo, Arlette Soudan-Nonault aliufungua mkutano huo ulioanza jana katika kituo cha mikutano nje kidogo ya mji mkuu Brazzaville na kuwakaribisha mamia ya wanamazingira, wanasayansi, makundi ya wannaharakati, viongozi wa kisiasa na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
Soma zaidi: Mkutano wa kilele wa msitu wa Amazon wafanyika Brazil
Washiriki hao wamekutana hasa kujadili mfumo wa ikolojia wa bonde la Kongo, Amazon na bonde la Borneo-Mekong la kusini mashariki mwa Asia. Kulingana na Waziri wa mazingira wa Kongo Arlette Soudan-Nonault, mabonde hayo matatu ya misitu ni asilimia 80 ya misitu yote ya kitropiki duniani na ina robo tatu ya viumbe hai vyake.
Ametabiri kuwa mkutano huo wa Kongo Brazzaville utatoa azimio thabiti la kanuni zinazokusudia kuendeleza rasilimali zinazothaminiwa za mabonde hayo makubwa matatu.
Ukataji miti bado ni tatizo kubwa kwenye misitu
Brazzaville ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza wa kilele wa aina hiyo mwaka 2011 ambapo washiriki walisaini tamko la ahadi ya kushirikiana katika mapambano dhidi ya ukataji miti. Tangu wakati huo kumekuwa na mikutano kadhaa, makongamano na matamko lakini tatizo la ukataji miti halijakomeshwa.
Katika ripoti iliyotolewa Jumanne wiki hii, mashirika yasiyo ya kiserikali na watafiti waligundua kuwa, dunia inashindwa kutekeleza ahadi ya kutokomeza ukataji miti hadi kufikia mwaka 2030, huku sehemu kubwa ya misitu ikiendelea kupotea kila mwaka.
Hata hivyo kiwango cha ukataji miti kwa mwaka 2022 kilikuwa zaidi ya asilimia 20 zaidi ya ilivyotarajiwa.
Tathmini iliyofanywa na makundi ya wanamazingira zaidi ya 20 na mashirika yanayofanya tafito yameonya pia kuwa uharibifu wa misitu unasalia kuwa tatizo kubwa.
Uharibifu huo ni wa aina nyingi na ni pamoja na moto wa nyikani na kupotea kwa viumbe hai, hali inayoathiri afya ya misitu kwa ujumla.