1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ukimwi wamalizika

28 Julai 2012

Mkutano wa 19 wa Kimataifa kuhusu Ukimwi umemalizika Washington, huku matumaini ya maendeleo katika tiba yakitandwa na wasiwasi wa ufadhili katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo uliowaathiri watu milioni 34 duniani.

https://p.dw.com/p/15fmy
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, akifunga mkutano wa kimataifa wa Ukimwi.
Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, akifunga mkutano wa kimataifa wa Ukimwi.Picha: AFP/Getty Images

Kiongozi wa chama cha Democratic katika bunge la Marekani, Nancy Pelosi, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kukata fedha zinazofadhili mapambano dhidi ya Ukimwi kutakuwa na gharama kubwa hapo baadaye katika maisha ya watu na hata fedha zenyewe.

Ufadhili wa kimataifa kwa utafiti na matibabu ya virusi vinavyosababisha Ukimwi na matibabu ya ugonjwa huo unakabiliwa na upungufu mkubwa katika wakati ambapo ulimwengu unasumbuliwa na mtikisiko wa kiuchumi na vile vile wasiwasi wa kukosekana kwa uwazi kwenye utafiti huo.

Wajumbe wataka uwazi zaidi

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambaye alizungumza kwenye ufungaji wa mkutano huo, alitaka kuwepo kwa matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa kupambana na Ukimwi.

Maandamano ya wanaharakati wa Ukimwi mbele ya Ikulu ya Marekani.
Maandamano ya wanaharakati wa Ukimwi mbele ya Ikulu ya Marekani.Picha: Reuters

"Baadhi ya washauri wa kimataifa wanalipwa hadi dola 600 kwa siku, wakati watu watatu wanaweza kutibiwa kwa kiwango hicho hicho cha fedha kwa mwaka mzima," alisema.

Clinton, ambaye wakfu wake unajihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi, alitaka kuongezeka kwa uwazi katika ufadhili, maamuzi ya ufadhili kufanyika kwa misingi ya kisayansi zaidi kuliko ya kisiasa na kuongezeka kwa uwajibikaji wa serikali na makundi ya misaada.

"Naamini serikali hata katika wakati huu mgumu zitafanya mengi zaidi ikiwa tutathibitisha kwamba tunaongeza matokeo ya kazi yetu maradufu." Alisema Clinton, akiongeza kwamba "ikiwa tutaendelea kutoa matokeo mazuri, fedha zitakuwepo."

Matokeo yanatia moyo

Taarifa zilizowasilishwa kwenye mkutano huo zilitoa matumaini ya kupatikana kwa tiba, ingawa watafiti waliepuka kutumia neno hilo kwenye mada zao, kwa mujibu wa gazeti la Washington Post la Ijumaa (27 Julai 2012).

Mwanamuziki Elton John akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi.
Mwanamuziki Elton John akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi.Picha: Reuters

Moja ya tafiti hizo ilihusishwa matumizi ya upandikizaji wa chembe hai wenye gharama kubwa kwa wagonjwa wawili waliokuwa wakitibiwa saratani ya damu, kwa mujibu wa Timothy Henrich na Daniel Kuritzkes wa Harvard Medical School.

Ugunduzi huo ulitiliwa nguvu na uzoefu wa Timothy Brown, raia wa Marekani ambaye alifanyiwa upandikizaji huo wa chembe hai kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu mjini Berlin, Ujerumani, kutoka kwa mtu ambaye alikuwa na kinga ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kuishi.

Brown alijitokeza hadharani mapema wiki hii katika mkutano huo kutangaza kwamba ametibika kutoka VVU kama matokeo ya dawa hiyo na akaanzisha kampeni ya kukusanya fedha kwa ajili ya utafiti zaidi. Asilimia moja ya watu wenye asili ya Caucasian duniani wana kinga hiyo.

Matokeo zaidi, matumaini zaidi

Utafiti mwengine ulionesha kwamba kundi la wagonjwa 14 nchini Ufaransa lilitibiwa VVU ndani ya wiki chache kutokana na vidonge na wakagundulika kutokuwa kabisa na VVU au kuwa na vichache sana miaka sita baadaye, kwa mujibu wa Charline Bacchus na Asier Saez Cirion wa Taasisi ya Pasteur ya Ufaransa.

Utolewaji wa Tunzo ya Elizabeth Taylor katika Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi.
Utolewaji wa Tunzo ya Elizabeth Taylor katika Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi.Picha: Getty Images

Utafiti wa tatu ulielezewa wiki hii katika jarida la Nature, ambao unahusisha kile kinachofahamika kama "kuamka" kwa chembe hai za VVU zilizolala na kujificha, ambazo zinaweza kugundulika na kuuliwa, kwa mujibu wa timu iliyoongozwa na David Margolis wa Chuo Kikuu cha Carolina ya Kaskazini.

Oliver Moldenhauer wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka amesema kwamba maendeleo katika mapambano dhidi ya Ukimwi ni wito unaodai hatua zichukuliwe haraka.

"Leo hii tunajuwa vyema zaidi kuliko hapo zamani namna ya kupambana na VVU/Ukimwi. Tunajua dawa gani za kutumia, matibabu gani ya kutumia katika vijiji vya mbali na namna ya kupunguza maambukizi mapya katika matibabu ya awali," alisema siku ya Alhamis (tarehe 26 Julai 2012). "Sasa tunapaswa kuchukua hatua."

Katika ufungaji wa mkutano huo, Rais Clinton alisoma ujumbe kutoka kwa raisi wa zamani wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandela, ambaye mwenyewe alikuwa kiongozi wa mapambano dhidi ya Ukimwi.

Clinton alisema kiongozi huyo wa miaka 94, ambaye mtoto wake wa kiume alikufa kwa ugonjwa unaohusiana na Ukimwi, alimuomba awaambie wanaohudhuria mkutano huo kwamba "Nimestaafu. Lakini nawatakia kila la kheri."

Mkutano wa 20 wa Kimataifa kuhusu Ukimwi utafanyika mjini Melbourne, Australia, mwaka 2014.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Bruce Amani