Mkutano wa kujadili amani ya Ukraine Uswisi utafanikiwa?
11 Juni 2024Mkutano huo wa viongozi mbalimbali wa ulimwengu utakaofanyika katika hoteli ya kifahari ya Burgenstock na ni mara tu baada ya mkutano wa kilele wa G7 uliofanyika kusini mwa Italia, ambapo nchi hizo pia zitajadili mzozo wa Ukraine mbele ya rais Volodymyr Zelensky.
Mataifa ya G7 kuanzia siku ya Alkhamisi hadi Jumamosi watajikita katika kuitazama namna ambavyo watatumia mali za Moscow zilizozuiliwa, ili kutoa msaada mpya kwa Ukraine ambayo ilivamiwa kijeshi na Urusi mnamo Februari 2022.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ataelekea nchini Uswisi kwa ajili ya kuungana na viongozi wengine kwa kile kinachotajwa kuwa "Mkutano wa kwanza wa Amani kuhusu Ukraine".
Soma pia:Zelensky apuuza taarifa za Urusi kuteka kijiji mkoani Sumy
Siku ya Jumatatu Rais wa Uswisi Viola Amherd aliwaambia wanahabari kuwa wanahitaji kuwa na mkakati mpana na endelevu kwa ajili ya kusaka amani ya Ukraine.
Alisema tukio hilo litaweka misingi katika mkutano wa kilele wa amani utakaohusisha moja kwa moja Urusi, kadhalika mkutano utaangazia mada zinazovuta nadhari ya kimataifa, ikijumuisha usalama wa nyuklia, usalama wa chakula na masuala ya kibinadamu.
"Matarajio juu ya mkutano huu yangali wazi. Tunataka kuanzisha mchakato mpana kuhusu amani endelevu na ya kudumu nchini Ukraine," rais Viola aliwaambia waandishi wa habari.
Aliongeza kwamba malengo hayo yana nia ya kutengeneza mazingiraya mkutano wa kilele wa amani kwa siku zijazo kwa uwepo wa ushiriki wa Urusi.
"Hilo litafanikiwa kwa mataifa kushirikiana." Alisema huku akisistiza ushiriki wa Urusi katika mkutano huo unatija kufikia mafanikio.
Moscow yaupuuza mkutano huo
Uswisi iliwaalika zaidi ya ujumbe 160 kutoka katika mataifa mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa.
Hadi sasa takriban mataifa na mashirika tisini yamejisajili kushiriki mkutano huo ambapo nusu yake ni mataifa ya Ulaya na karibu asilimia 50 kati ya mataifa yatawakilishwa na wakuu wa nchi au serikali.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida ni miongoni mwa waliothibitishwa kuhudhuria hadi sasa.
Hata hivyo serikali ya mjini Moscow ambayo haijaalikwa kushiriki mkutano huo imepuuzilia mbali mpango huo na kusema ni upotezwaji wa muda.
Soma pia:Scholz arejelea uungaji wake mkono kwa Ukraine kabla ya uchaguzi wa EU
Uswizi inasema haikuialika Urusi kutokana na kutoonesha kwake nia ya kushiriki katika mkutano huo, lakini inasisitiza kuwa ni muhimu Urusi kuwa sehemu ya mchakato wa amani.
Kutokuwepo kwake kumetoa himizo kwa washirika wa Moscow wenye nguvu kama vile China
Beijing ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi imesema kuwa hakuna maana kuwepo kwa mchakato wa amani pasina ushiriki kamilifu wa pande zote za mzozo, Urusi na Ukraine.
Matamshi hayo yanatafsiriwa na wachambuzi na wafuatiliaji wa mzozo huo huwa, huenda ukazima matarajio chanya kufuatia mchakato huo.
Kyiv yatarajia uungwaji mkono zaidi wa kimataifa
Mkutano huo ambao umeandaliwa kufuatia ombo la Kyiv matokeo yake bado hayajajulikana ingawaje, Uswis inalo tumaini katika tamko la pamoja baada ya mkutano huo.
Ukraine inataraji kupata uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa katika masharti yake ya kukomesha vita vilivyoingia mwaka wake wa tatu.
Hata hivyo moja wa afisa katika serikali ya Ujerumani ambae hakutaka jina lake kutajwa alisisitiza kuwa ni muhimu mno kwa kutokuweka matarajio yaliokithiri na badala yake kuweka suluhu ya amani ya kudumu katika mzozo huo uliogharimu masiha ya maelfu ya watu na wengine mamilioni kuyakimbia makaazi yao, huku miondombinu muhimu ikiharibiwa vibaya.
Soma pia:Ufaransa itaanza mara moja kuwafundisha wanajeshi wa Ukraine kutumia ndege za kivita za Mirage
Ikulu ya Kremlin imesisitiza mara kwa mara kwamba haitashiriki katika mazungumzo yoyote yenye kunuia kupata suluhu ya vita hivyo, ikiwa Kyiv haitakubali Moscow kutwaa takriban asilimia 20 ya eneo la Ukreine ambalo Urusi inakalia hivi sasa.