1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kutafuta amani ya Burundi waahirishwa

24 Oktoba 2018

Mazungumzo ya amani ya Burundi yameahirishwa hadi kesho Alhamisi kwa kile kilichotajwa na makundi ya upinzani kuwa ni kuishinikiza serikali kushiriki katika mazungumzo yanayoongozwa na Benjamen Mkapa.

https://p.dw.com/p/377Gs
Der frühere Präsident Tansanias Benjamin Mkapa
Picha: Abbas Mbazumutima/Iwacu

Hadi kufikia mchana wa leo makundi yote ya upinzani na wanaharakati wa Burundi walioko uhamishoni walikuwa tayari katika hoteli ya Ngurdoto yapata kilomita ishirini na tano kutoka Jijijni Arusha tayari kushiriki katika mazungumzo hayo ya amani ya awamu ya tano.

Baadhi ya wanaharakati wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina wanasema kuwa mazungumzo hayana maana yoyote ikiwa serikali ya Burundi haitatuma wawakilishi wake kujadili mustakabali wa taifa hilo ambalo limekuwa katika hali tete kwa miaka kadhaa sasa.

Hata hivyo ofisi ya msuluhishi wa mgogoro huo haijatoa taarifa rasmi iwapo madai hayo ndio chanzo cha kuahirishwa kwa ufunguzi rasmi wa mazungumzo hayo. 

Präsident Burundi Pierre Nkurunziza
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza Picha: Imago/photothek/U. Grabowski

Naye rais wa chama cha UPD zigamibanga Chauvineau Mugwengezo amesema hatua ya serikali ya Burundi kushindwa kushiriki katika mazungumzo hayo kwa kigezo cha kusema kuwa inaomboleza vifo vya waasisi wa taifa hilo waliopoteza maisha miaka mingi ni porojo na inaonyesha jinsi ambavyo serikali ya Bunjumbura inavyoyapuuza mazungumzo hayo.

Tangu mazungumzo hayo ya kusaka amani ya Burundi yaanze miaka mitatu iliyopita pande zinazopigana katika mgogoro huo hazijawahi kukutana uso kwa uso na msuluhishi rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa amekuwa akikutana na makund tofauti kwa nyakati tofauti kwa lengo la kuleta upatanisho miongoni mwa Warundi.

Mwandishi: Charles Ngereza DW Arusha

Mhariri: Iddi Ssessanga