Mkutano wa kwanza wa mawaziri wa UAE na Israel mjini Berlin
6 Oktoba 2020Mkutano wa pili ni wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel na kiongozi wa upinzani wa Belarus Svetlana Tikhanovskaya.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas atawapokea Gabi Ashkenazi waziri wa mambo ya kigeni wa Israel pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Emirati Abdullah bin Zayed al-Nahyan mchana wa leo.
"Ni fahari kubwa kwamba mawaziri wa mambo ya kigeni wa Israel na Emirati wamechagua Berlin kuwa sehemu ya mkutano wao wa kwanza wa kihistoria," amesema Maas katika taarifa kabla ya mkutano huo, akiwashukuru wenzake hao kwa kuiamini Ujerumani.
Makubaliano "ya kijasiri ya amani " kati ya Israel na Emirati yalikuwa ni habari nzuri za kwanza katika Mashariki ya Kati kuwahi kutokea kwa muda mrefu na wakati huo huo ni fursa ya vuguvugu jipya katika majadiliano kati ya Waisraeli na Wapalestina , amesema.
Maas ana matumaini , "kwamba Berlin itatoa fursa nzuri kwa hatua zaidi za majadiliano katika mwelekeo huo."
Mkutano huo unakuja baada ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa UAE na Bahrain kukamilisha uanzishwaji wa mahusiano ya kibalozi na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hapo Septemba 15.
Tikhanovskaya
Utiaji saini ulifanyika mbele ya rais wa Marekani Donald Trump katika ikulu ya White House mjini Washington.
Kwa upande wake kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kukutana na kiongozi wa upinzani nchini Belarus Svetlana Tikhanovskaya. Akizungumza na gazeti la Der Spiegel kabla ya mkutano huo, Tikhanovskaya alionesha kuwa majadiliano yanaweza kujumuisha uwezekano wa kansela kufanya upatanishi katika mzozo huo nchini mwake.
Rais wa muda mrefu wa Belarus Alexander Lukashenko anaendelea kuwa madarakani mjini Minsk licha ya kukataliwa na Ujerumani na mataifa mengi mengine katika uchaguzi wa hapo Agosti, ambapo alidai kupata ushindi wa kishindo.
Tikhanovskaya alikuwa wa pili katika uchaguzi huo, kwa mujibu wa matokeo rasmi ya jumla.
Waungaji wake mkono wanadai kuwa ameshinda uchaguzi huo. Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert , amesema kansela anasubiri kwa hamu mkutano huo na amesisitiza uungaji mkono wa Ujerumani wa maandamano ya amani ya kupinga serikali nchini Belarus.
mara baada ya kukutana na Merkel , Tikhanovskaya anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vya Green mjini Berlin. Kesho Jumatano anatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas.