1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi Paris

10 Desemba 2015

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaendelea Le Bourget. Mawaziri wa mataifa 195 wanalazimika kusawazisha misimamo ya nchi za kusini na zile, za kaskazini, wakitaka kufikia makubaliano ijumaa, kama ilivyopangwa.

https://p.dw.com/p/1HL8v
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ufaransa akihutubia wajumbe katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi COP21Picha: Reuters/S. Mahe

Mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi unaendelea Le Bourget ,karibu na Paris. Mawaziri wa mataifa 195 wanalazimika kusawazisha misimamo ya nchi za kusini na zile,za kaskazini,wakitaka kufikia makubaliano kesho ijumaa, kama ilivyopangwa.

Pindi wakikubaliana hayo yatakuwa makubaliano ya kimataifa yatakayozuwia majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, yanayoshuhudiwa kila kukicha.

Zikiwa zimesalia chini ya saa 36 kabla ya muda uliowekwa kukamilika,mkutano huo wa Le Bourget unaonyesha unazorota katika masuala matatu muhimu-na majadiliano ya jana usiku yamebainisha njia ya kufikia makubaliano imejaa vizingiti.

Fabius awapa moyo wajumbe mkutanoni

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius,ambae ndie mwenyekiti wa mkutano huo unaojulikana kama COP21,aliwakabidhi wajumbe 196 mswaada wa waraka,uliofupishwa na ambao takriban nusu ya vifungu vyake vinaonyesha viko tayari kuratibiwa."Ni waraka mfupi wa kurasa 29 badala ya 43,ukijumuishwa mswaada wa makubaliano na uamuzi uliopitishwa na COP21. Na kulinganisha na waraka wa awali,vifungu ambavyo vinasubiri ufafanuzi vimepungua kwa kadiri asili mia 75. Kwa hivyo kishindo kimepungua sana,ingawa bado ni kikubwa."Amesma Fabius.

Frankreich Cop21 Klimagipfel in Paris - Faces of Climate Change - Kumi Naidoo
Wajihi wa Mabadiliko ya tabianchiPicha: DW/T. Walker & R. Krause

Miongoni mwa mada zinazobidi kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na jinsi ya kugharimiwa miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi baada ya mwaka 2020,na vipi kutekeleza mwongozo "kuhusu jukumu la pamoja lakini kwa viwango tofauti."

Kabla ya duru ya mazungumzo jana usiku,wawakilishi wa nchi hizo zinazoinukia walielezea msimamo wao wakipinga kuwekwa mstari mmoja na nchi za kaskazini,wanazosema zinabeba jukumu la jadi la kuongezeka hali ya joto duniani na ambazo wanasema zenye uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na majanga kama hayo.

Waraka unakosolewa na wawakilishi wa nchi zinazoinukia

"Makubaliano ya kudumu hayawezi kupatikana kwa kufifiisha jukumu la kihistoria na kwa kuwatumbukiza ndani ya chungu kimoja wachafuzi na wahanga wa uchaguzi-"Amesema Prakash Javadekar-waziri wa mazingira wa India ambae nchi yake inashikilia nafasi ya mbele katika mazungumzo ya Le Bourget.

BdW Global Ideas Bild der Woche KW 49/2015 Perito Moreno Eisberg
Milima ya barafu huko Santa Kruz-Argentina yaanza kuyayukaPicha: Getty Images/M. Tama

Akiwakabidhi mswaada wa makubaliano waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius aliwahimiza wajumbe mkutanoni waridhiane kuhusu mswaada mpya hadi ifikapo leo jioni.Makubaliano kamili yanatarajiwa kesho jioni.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman