Mkutano wa Singapore bado wajadiliwa
13 Juni 2018Gazeti la Stuttgarter Nachrichten
Bado kuna wasiwasi ikiwa kuna kilichoachwa kufuatia mkutano wa siku moja kati ya rais wa Marekani na Dikteta wa Korea Kaskazini nchini Singapore zaidi ya picha za viongozi hao wawili kwa ajili ya kitabu cha kumbukumbu.Pamoja na hilo inawezekana kuwa ni mwanzo wa mchakato wa mazungumzo ya amani. Lakini juu ya yote kukutana kwa viongozi hao ni bora zaidi kuliko yaliyokuwa yakishuhudiwa miezi ya karibuni,kurushiana vijembe,kutukanana,kuchokozana na kutishia kushambuliana.
Gazeti la Sächsische Zeitung
Ahadi ya bwana Kim kwamba ataondowa kabisa silaha za Nyuklia inaonesha kama ni ujasiri unaotia moyo. Lakini kinachopaswa kueleweka ni kwamba hakuna kinachomfunga Dikteta huyo kutimiza alichoahidi kwa sababu hakuna sehemu yoyote lilikotolewa tamko la kumlazimisha na wala hakuna muda wowote uliowekwa wa kutimiza ahadi yake. Mkutano wa Singapore umelifikia lengo dogo tu,nalo ni kufungua mchakato wa mazungumzo yatakayopelekea uwezekano wa kuondolewa kwa silaha za Nyuklia katika rasi ya Korea na kupatikana makubaliano ya amani. Hata hivyo kwa hili mtu huwezi kuwa na ndoto. Inawezekana ikachukua miaka chungunzima. Na ikiwa kilichofikiwa katika mkutano kitaendelea kuheshimiwa hilo peke yake ni jambo linalowekewa masuali.
Gazeti la Braunschweiger kuhusu kuzuiwa meli ya wakimbizi ya Aquarius.
Kwa wataliana kupoteza taratibu subira,hilo mtu anaweza kulielewa. Na kitendo cha serikali yao mpya ya mrengo wa kulia ya chama cha Liga na vuguvugu la siasa kali za kizalendo la nyota tano cha kuizuia meli ya Aquarius kutia nanga pia ni matokea yaliyosababishwa na sera mbaya iliyoshindwa ya Ulaya kuhusu wakimbizi. Na kwa hivyo kiongozi wa chama cha Liga ambaye ni waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini anasema kuwaokoa watu baharini wanaohitaji msaada wa haraka sio suluhisho. Kwa maneno mengine anachomaanisha ni kwamba hata mtu wa zima moto anapookowa watu kwenye nyumba inayoteketea anafanya kitu kisichokuwa cha kawaida. Lakini hilo halimaanishi kwamba kila aliyeachwa bila sehemu ya kuishi baada ya nyumba kuteketea hatimae anapaswa kukaa kwa zima moto. Kimsingi yuko sawa na inaingia akilini.
Gazeti la Markische Oderzeitung kuhusu Ujerumani na mgogoro wa sera ya wakimbizi.
Mvutano wa zamani umeibuka tena na mara hii huenda ukafikia mahala pabaya. Kadhia iliyoikumba idara ya uhamiaji na wakimbizi ni suala linalohitaji haraka kutolewa ufafanuzi. Wananchi wenye wasiwasi bado wanasubiri kupata majibu kuhusu kisa cha kuuliwa msichana Sussana. Na kama haitoshi si tu masuala haya yanaweza kuilemaza serikali ya muungano lakini yanaweza hata kuiporomosha kabisa.
Na taarifa hiyo ndio inahitimisha yale yaliyoandikwa na wahariri wa magazeti ya hapa Ujerumani yaliyokusanywa na Saumu Mwasimba
Mwandishi :Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo