1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Ujerumani na Uturuki kupunguza mivutano

Sekione Kitojo
6 Januari 2018

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Sigmar Gabriel Jumamosi(06.01.2018)atakuwa mwenyeji wa waziri mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglo kwa mazungumzo wakati nchi hizo mbili zikijaribu kumaliza mzozo wa tofauti zao.

https://p.dw.com/p/2qQFl
Türkei Ankara Sigmar Gabriel trifft Mevlut Cavusoglu
Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Mahusiano kati ya  washirika  hao  wa  jumuiya  ya  kujihami  ya NATO yamevurugika  kwa  kiasi  kikubwa , hususan  tangu  pale lilipofanyika  jaribio  lililoshindwa  la  mapinduzi  nchini  Uturuki mwaka  2016 na  kuanza  ukandamizaji  ambao ulishuhudia  mamia kwa maelfu  ya  watu  wakikamatwa, ikiwa  ni  pamoja  na Wajerumani  kadhaa  ama  wale  wenye uraia  pacha.

Sigmar Gebriel
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Sigmar GabrielPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Ujerumani  ambayo  ina  wakaazi  milioni tatu wenye  asili  ya Uturuki , mwaka  jana iliwashauri  wawekezaji  wake pamoja  na Wajerumani  wanaokwenda  Uturuki  kwa  ajili  ya  mapumziko  ya likizo  kuepuka  kwenda  nchini  humo  na  kutaka  kupunguzwa  kwa fedha zinazotolewa  kwa  Uturuki  kutoka  katika  Umoja wa  Ulaya zinazohusishwa  na  mazungumzo  yaliyokwama  ya  uanachama.

Hata hivyo , Uturuki katika wiki  za  hivi  karibuni  imetuma ishara kadhaa kwamba  inataka  kurejea  katika  mahusiano  bora  na Umoja  wa  Ulaya  na  Ujerumani, katika  wakati  ikiwa  katika uhusiano  tete  na  Marekani, Israel  na  baadhi  ya   mataifa  ya ghuba.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan , kwa  kutangaza mwezi uliopita kwamba  Uturuki "inalazimika  kupunguza idadi ya  maadui zake  na  kuongeza idadi  ya  marafiki", alikutana  na  rais Emmanuel Macron  wa  Ufaransa  mjini  Paris  Ijumaa(05.01.2018).

Frankreich Treffen Macron und Erdogan
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kushoto) na rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: picture alliance/abaca/Somer

Akiongeza  uhusiano wa binafsi  katika  mazungumzo  ya  Jumamosi, Gabriel amemwalika  waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Uturuki katika  mji  anakotoka  wa  Goslar, baada  ya  viongozi  hao  wawili kukutana  mwezi  Novemba  katika  mji  anakotoka Cavusoglo katika jimbo  la  kusini  la  Antalya.

Matembezi ya pamoja

Kufuatia  taarifa  za  vyombo  vya  habari  jana, Gabriel atamchukua mgeni  wake  kwa  matembezi  katika  mji  wa  kale ambao umeorodheshwa  kuwa ni  turathi  wa  Goslar , ulioko   karibu  na brunswick katika milima  ya  Harz.

Casovuglo  katika  uhariri  wa  gazeti jana Ijumaa  ametaka kumalizika  kwa kile  alichokiita "diplomasia  ya kupigizana kelele" baina ya  Uturuki  na  Ujerumani  na  kuanza "mwanzo  mpya" ulio katika  msingi  wa  urafiki  na  ushirikiano  kati ya "washirika sawa".

Ujerumani  pia  ilitaka ukaribiano  wa "hatua  kwa  hatua"  na kusema  mazungumzo  ya  Jumamosi yataangalia  masuala  kadhaa ikiwa  ni  pamoja  na "matatizo", msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya kigeni  amesema.

Journalist Deniz Yücel (Ausschnitt)
Mwandishi habari Deniz Yücel ambaye yuko kizuwizini nchini UturukiPicha: picture-alliance/Eventpress/Stauffenberg

Kikwazo  kikubwa  hivi  sasa  ni  kuwekwa  kizuwizini  kwa mwandishi  wa  gazeti  la  Die Welt mwenye uraia  wa  Uturuki  na Ujerumani  Deniz Yecel  kwa  madai  ya  ugaidi  tangu  Februari mwaka  jana, na  Wajerumani  wengine  sita  ambao  serikali inasema  wamefungwa  kwa "sababu  za  kisiasa".

Uturuki  katika  wiki  za  hivi  karibuni  imewaachia  huru  Wajerumani kadhaa  ambao  Gabriel amewaeleza  kuwa  ni "mateka", miongoni mwao  ni  mwandishi  habari Mesale Tolu.

Matumaini yaongezeka kwa watu walioko kizuwizini

Matumaini  yameongezeka  kwamba  kesi  ya  Yucel  pia inaweza kutatuliwa  baada  ya  serikali  ya  Uturuki  wiki  hii kuishughulikia kwa  mara  ya  kwanza  katika  miezi  10 kwa  kuipeleka  katika mahakama  ya  katiba, ambayo  hivi  karibu  itaamua  iwapo kumwachia  kutoka  katika kizuwizi  cha  kabla  ya  kuanza  kwa  kesi.

Casovuglo amesisitiza  uhuru wa  mahakama  za  Uturuki  lakini ameahidi  kwamba "tunafanya kila  liwezekanalo katika  madaraka yetu  ya  kisiasa   kuharakisha  mahakama  kuchukua  hatua".

Türkei Außenminister Mevlut Cavusoglu
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: picture-alliance/dpa/A. Deeb

Mzozo  kati  ya  nchi  hizo  mbili  katika  miaka  ya  hivi  karibuni umechochewa na  mizozo  mingine, kuhusiana  na mchekeshaji  wa televisheni  ya  Ujerumani  alipomkashifu  Erdogan, azimio  la  bunge la  Ujerumani  mwaka  2016  kuhusiana  na  mauaji  ya  kimbari  ya Warmenia, na  Uturuki  kukataa  ziara  zilizokuwa  zifanywe  na wabunge  wa  Ujerumani  katika  vituo  vya  kijeshi  nchini  Uturuki.

Uturuki  imeishutumu  Ujerumani  kwa  kushindwa  kuwakamata wafuasi  imamu  anayeishi  Marekani  Fethullah Gulen , ambayo  nchi hiyo  inamshutumu  kwa  kuhusika  na  jaribio  la  mapinduzi  la mwaka  2016, na  kushindwa  kuwazuwia wanamgambo  wa  Kikurdi.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi