1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa umoja wa Afrika UA

Kitojo, Sekione1 Julai 2008

Viongozi wa mataifa ya Afrika wazungumzia kuhusu Zimbabwe leo katika mkutano wa faragha, mjini Sharm El-Sheikh

https://p.dw.com/p/EU7Z
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe akihudhuria mkutano wa umoja wa Afrika mjini Sharm El-Sheikh nchini Misr hivi karibuni.Picha: AP



Viongozi wa mataifa ya Afrika wameanza mazungumzo yao leo kuhusiana na vipi wanaweza kushughulika na suala la rais Robert Mugabe wa Zimbabwe wakati Marekani na umoja wa mataifa unajitayarisha kuweka vikwazo kutokana na uchaguzi uliofanyika nchini humo ambapo alikuwa mgombea pekee , wakati jumuiya ya kimataifa nayo imeueleza kuwa ni kichekesho tu.




Umoja wa Afrika wenye wanachama 53 umekuwa ukifanya mkutano wake kwa faragha katika siku ya mwisho ya mkutano wao nchini Misr huku kukiwa na mbinyo mkali kwa viongozi wa bara hilo kuchukua hatua kuutatua mzozo ambao baadhi wanahofia kuwa unaweza kudhoofisha eneo la kusini mwa Afrika.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameahidi kutoa msaada wa upatanishi, akirudia mawazo yake kuwa uchaguzi uliokuwa na ghasia ambao umempa kiongozi mkongwe Robert Mugabe nafasi nyingine ya kutawala kuwa haukuwa na uhalali.

Ban amesema kuwa Wazimbabwe wanapaswa kufurahia uhuru halisi, ili waweze kuwa katika nafasi nzuri ya kuchagua kiongozi wao kutokana na matakwa yao bila ya kutishwa.

Hali nchini Zimbabwe inahusisha mambo mengi sio tu kwa watu na serikali ya Zimbabwe, Ban amesema , na kuita hali hiyo , muhimu kwa ajili ya kuendeleza hali ya kuaminika kwa utawala wa demokrasia katika bara zima la Afrika kwa jumla.

Baadhi ya viongozi wa Afrika wamedai kuchukuliwa hatua kali dhidi ya Mugabe. Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga ametaka rais huyo wa Zimbabwe kuondolewa kutoka katika mkutano huo wa mataifa ya Afrika hadi pale atakaporuhusu uchaguzi huru na wa haki.

Lakini kwa upande mwingine, kiongozi aliyetawala kwa muda mrefu zaidi katika bara hilo rais Omar Bongo wa Gabon , amesisitiza kuwa viongozi wa Afrika wanapaswa kukubali ushindi wa rais Mugabe.

Amesema kuwa Mugabe amechaguliwa na ameapishwa, na yuko hapa nasi, kwa hiyo ni rais na hatuwezi kudai zaidi kutoka kwake, Bongo amewaambia waandishi wa habari jana Jumatatu.

Mugabe mwenye umri wa miaka 84, aliapishwa kwa kipindi cha sita katika utawala wake baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika siku ya Ijumaa wa duru ya pili ambapo mgombea wa chama cha upinzani Morgan Tsvangirai alisusia kutokana na ghasia pamoja na kutishwa kwa wapigakura.

Mugabe akihudhuria mkutano huo wa siku mbili, anatarajia kusikia shutuma zaidi dhidi yake na miito ya kupatiwa suluhisho mzozo huo, ikiwa ni shutuma kama hizo alizosikia katika ufunguzi wa mkutano huo jana Jumatatu kutoka kwa naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Asha Rose Migiro.

Wakati huo huo gazeti moja la Afrika kusini limeripoti leo kuwa nchi hiyo iko karibu na kupata makubaliano ambayo yatawaweka pamoja rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kujadili juu ya serikali ya umoja wa kitaifa.

Mpango huo gazeti hilo la Business Day limesema unahusisha kumuweka pamoja Mugabe na Tsvangirai ili kutekeleza makubaliano baina ya ZANU-PF na chama cha Movement for Democratic Change yaliyofikiwa mwezi Januari. Hii ikiwa ni pamoja na katiba mpya na mageuzi mengine.

►◄