Miji mingi nchi zinazoendelea haijapangiliwa
18 Oktoba 2016Ban ameyasema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu makaazi na maendeleo endelevu kwenye maeneo ya mijini unaofahamika kama Habitat 3.
Mkutano huo ambao utaendelea mpaka siku ya alhamis wiki hii, una lengo la kujadili jinsi ya kushugulikia ongezeko la watu maeneo ya mijini katika miaka 20 ijayo. Unafanyika katika mji mkuu wa Equador, Quito ambapo wawakilishi kutoka miji 180 wanahudhuria, ukiwa ni mkutano wa tatu kuhusu maakazi baada ya ule wa mwaka 1976 na 1996
Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka 20 unafanyika kwa mara ya kwanza kukiwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi maeneo ya mijini ukilinganisha na vijijini
Peter Thomson, rais wa baraza la usalama la umoja wa mataifa amesema kuwa watu bilioni moja wanaishi katika maeneo ya mijini yaliyo na msongamano mkubwa ambako hakuna upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii kama vile upatikanaji wa maji safi na salama na nishati ya umeme yenye uhakika, na kuongeza kuwa kuna ongezeko kubwa la miji isiyopangiliwa hasa katika nchi zinazoendelea
Upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, kuwepo kwa maeneo ya kutosha kuishi, kuwa mbali na maeneo ya kazi, kuwa katika hatari ya uhalifu na kulazimishwa kuhama makaazi ni baadhi ya mambo ambayo yanahitaji kushughulikiwa kwa haraka.
''Asilimia 70 ya miji ina kiwango kikubwa cha pengo la kipato miongoni mwa wakzi wake kuliko ilivyokuwa mwaka 1996, na asilimia 70 ya hewa inayochafua mazingira ina chanzo chake katika maeneo ya mijini'', amesema Peter Thompson, mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya watu 45, 000 wakiwa ni wawakilishi wa Serikali, mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, wanasayansi wataalamu wa mipango pamoja na maafisa wa umoja wa mataifa wanahudhuria mkutano huo kujadili mustakabali wa miji duniani. Inakadiriwa kuwa karibu wanachama 140 wa umoja wa mataifa watachukua hatua mpya za makubaliano ya kuthibiti ukuaji wa miji, maarufu kama New Urban Agenda-NUA.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/ AP/DPA/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel