1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa usalama Munich: Je diplomasia imefikia ukingoni?

19 Februari 2018

Baada ya siku tatu za majadiliano, jambo moja lilijitokeza wazi. Mgogoro. Mkutano huo ulikumbwa na hali ya kunyosheana vidole au kulaumiana. Mafanikio kamili yalikuwa nadra kupatikana

https://p.dw.com/p/2sukL
Münchner Sicherheitskonferenz Mohammed Dschawad Sarif
Picha: picture alliance/dpa/S. Hoppe

Kiutamaduni, mkutano wa usalama wa Munich huakisi hali halisi ya usalama. Lakini mwaka huu, mkutano huo ulikumbwa na hali ya kunyosheana vidole au kulaumiana. Mafanikio kamili yalikuwa nadra kupatikana. Ni maoni yake mwandishi wa habari wa DW Mathias von Hein.

Kulikuwa na miaka ambapo Mkutano wa Usalama wa Munich ulitoa ishara ya maelewano na matumaini. Hayo hayakujitokeza katika awamu hii ya 54. Kauli mbiu  ya mwaka huu je ilikuwa ni "kufikia ukingoni na kurudi tena?" Kwa hakika hiyo ndiyo iliyoonekana kuwa tafrisiri kamili ya hali ambayo dunia imejikuta kwa sasa.

Baada ya siku tatu za majadiliano, jambo moja lilijitokeza wazi. Hali zote ziliashiria mgogoro uliothibitisha swali la kauli mbiu. Kwa mara nyingine mkutano huo ulithibitisha kuwa ni mahali ambapo matatizo mengi yanayoikabili dunia hutajwa, hujadiliwa na kutathminiwa.

Mwanadiplomasia Wolfgang Ischinger
Mwanadiplomasia Wolfgang IschingerPicha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Lakini kilichojitokeza ni kwamba diplomasia imefikia ukingoni. Japo kiongozi wa mkutano huo Wolfgang Ischinger anastahili kupongezwa kwa kuwaleta wawakilishi kutoka kambi tofautitofauti katika jukwaa moja, mkutano wenyewe ulionekana kugeuzwa  kuwa jukwaa la kusigana, kutofautiana sambamba na kuwepo misimamo iliyotengana na isiyoweza kusawazishwa. Waliotarajia kuona ishara za maelewano, na mapendekezo muhimu ya kusuluhisha masuala tete waliambulia patupu.

Benjamin Netanyahu aionya Iran

Malumbano ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na mwenzake kutoka Saudi Arabia Adel bin Ahmed Al-Jubeir katika siku ya mwisho ya mkutano huo, yalirejesha kumbukumbu za kauli zilizotolewa katika mkutano wa mwaka uliopita. Hali hiyo imeonesha wazi ishara ya kwamba hali haiwezi kudhibitiwa kiurashisi.

Hata kiongozi wa mkutano huo Ischinger kama mwanadiplomasia alikiri kuwa wahusika hawakuwa na hatua madhubuti za kusuluhisha matatizo ya kiusalama yanayoikumba dunia.

Mfano mwengine ni hatua ya kutaka Uturuki kumuachia huru mwandishi wa habari wa Ujerumani Deniz Yücel, kutawala mijadala ya pembezoni katika siku ya kwanza ya mkutano huo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa/MSC 2018/L. Preiss

Maneno makali katika mkutano

Kutoweka kwa diplomasia ya kuchagua maneno ya kuzungumza hadharani ni suala lililodhihirishwa na rais wa Poland Mateusz Morawiecki. Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu sheria mpya wa Poland kuhusu mauaji ya kimbari ya Wayahudi Holocaust, alikiri kuwa kuna Wapoland waliowapinga Wayahudi na walifanya makosa ya jinai dhidi yao wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia. Kisha akaongeza kwa kusema kama ambavyo ilionekana kwa baadhi ya Wayahudi, Warusi na Waturuki na sio tu baadhi ya Wajerumani.

Mahusiano magumu kati ya nchi za Magharibi yalitawaliwa na kutosameheana na kulaumiana badala ya diplomasia. Rais wa Ukraine Petro Poroshenko aliielezea Urusi kama chanzo cha matatizo yote yanayoikumba Ulaya. Alitaka shinikizo zaidi dhidi ya Urusi na akapinga kulegezwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi huku akielezea nia yake ya kutaka Ukraine ijumuishwe haraka iwezekanavyo katika Umoja wa Ulaya na katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel akihutubia mkutano wa usalama Munich
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel akihutubia mkutano wa usalama MunichPicha: Getty Images/AFP/T. Kienzle

Mara kwa mara Ulaya imelalamikia suala la diplomasia kukosa maana kwa Marekani katika siku za hivi karibuni. Hali ambayo imedhihirika wazi kufuatia hatua ya utawala wa Trump kupunguza bajeti ya mambo ya nje. Swali lao ni je wanapaswa hata kuzungumza? Na ikiwa mazungumzo yanafanywa tu kwa misingi ya uwezo wa kijeshi, basi hayana maana bali ni udikteta.

Mwandishi: Mathias von Hein

Imetafsiriwa na: John Juma

Mhariri: Yusuf Saumu