Mkutano wa wafadhili wa Palestina wafanyika Paris
17 Desemba 2007Umoja wa Ulaya unatarajiwa kuahidi msaada ya karibu euro milioni 450 kwa Wapalestina kwenye mkutano wa wafadhili ulioanza leo mjini Paris, Ufaransa.
Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na uhusinao wa nchi za kigeni, Benita Ferrero Waldner, ameyasema hayo kabla mkutano huo wa mjini Paris kuanza.
Ujerumani imesema itatoa euro milioni 200 kufikia mwaka wa 2010 kusaidia miradi ya maendeleo inayosimamiwa na mamlaka ya Palestina.
Mkutano huo wa kimataifa unaowaleta pamoja wafadhili mbalimbali, unalenga kusaidia juhudi za kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina na kuuongezea nguvu mchakato wa amani uliofufuliwa hivi majuzi kati ya Palestina na Israel.
Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, anahitaji kiasi cha euro bilioni 3.86 kwa ajili ya mpango wake wa miaka mitatu unaolenga kuufua uchumi wa Palestina.
Wakati haya yakiarifiwa, Japan imeahidi itatoa dola milioni 150 kwa Palestina. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Japan, Masahiko Komura, amesema mkutnao wa mjini Paris unatoa nafasi ya kihistoria kuweza kuunda taifa huru la Palestina litakaloishi kwa amani na Israel.