1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Volker Turk wa UN atoa mwito wa haki kuzingatiwa Syria

15 Januari 2025

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk amesema mchakato wa kutafuta haki katika kipindi cha utawala wa mpito nchini Syria ni muhimu kwa taifa hilo, baada ya kuangushwa kwa utawala wa Bashar al Assad.

https://p.dw.com/p/4pB33
Kamishna wa haki za binadamu wa UN Volker Turk
Kamishna wa haki za binadamu wa UN Volker TurkPicha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ametoa wito Jumatano kwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa nchini Syria ili kuhakikisha haki inapatikana kwa uhalifu uliofanywa katika kipindi cha miongo mitano ya utawala wa mabavu wa familia ya Assad.

Rais Bashar al-Assad aling’olewa madarakani mwezi uliopita kufuatia mashambulizi ya ghafla ya waasi, na hivyo kumaliza miaka 54 ya utawala wa familia yake na kuibua matumaini ya kuwajibika kwa uhalifu uliofanyika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu zaidi ya miaka 13 nchini Syria.

Soma pia: UN: Wasyria wanaorejea nyumbani wanakabiliwa na unyanyasaji

Katika ziara ya kwanza kabisa ya kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa mjini Damascus, Turk alikutana na mkuu wa utawala mpya wa Syria, Ahmed al-Sharaa, pamoja na waathiriwa wa uhalifu wa vita.

"Haki ya mpito ni muhimu Syria inapopiga hatua mbele," Turk aliwaambia waandishi wa habari Damascus. "Kisasi na kulipiza kisasi siyo suluhisho. Badala yake, kunahitajika mchakato wa kitaifa wa uponyaji, kusema ukweli, na maridhiano."

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW