1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa Sera wa EU azuru Myanmar

28 Aprili 2012

Mkuu wa Sera za Umoja wa Ulaya Catherine Ashton yuko nchi Mynamr leo kwa lengo la kufungua ukurasa mpya wa mahusiano kufuatia ulegezaji wa vikwazo vilivyowekewa nchi hiyo unaotarajiwa kuimarisha uwekezaji nchini humo.

https://p.dw.com/p/14mLg
Catherine Ashton Mkuu wa Sera wa Umoja wa Ulaya
Catherine Ashton Mkuu wa Sera wa Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa

Ziara hiyo ya Ashton ni ya kwanza kwa kiongozi wa Umoja wa Ulaya nchini humo tangu wanajeshi walipoupindua utawala wa kiraia na kusababisha kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na jumuiya mbalimbali za kimataifa.

Uondoaji wa vikwazo ulilenga kuwezesha misaada na uwekezaji kuingia nchini humo kama zawadi kwa kitendo cha nchi hiyo kuanza kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi lakini pia mambo yanaweza kubadilika wakati wowote na vikwazo kurejea endapo mchakato huo wa kurejesha demokrasia utasitishwa na nchi hiyo.

Wito wa mabadiliko zaidi

Vyombo vya habari vimemnukuu Ashton wakati wa ziara yake hiyo akisema ni lazima mabadiliko hayo yaendelee na wanahitaji kuona maendeleo zaidi ya mchakato huo.

Myanmar imesifiwa kwa mabadiliko ya kisiasa hivi karibuni
Myanmar imesifiwa kwa mabadiliko ya kisiasa hivi karibuniPicha: reuters

"Tupo tayari kuiunga mkono Myanmar katika mchakato wake huu kuelekea demokrasia na hata katika nyanja za uchumi na maendeleo ya jamii. Tutaendelea kusaidia mabadiliko haya ya kisiasa ili yawe na mafanikio ikiwemo kutoa msaada wakati wa chaguzi, pamoja na kihimiza uwekezaji na biashara kwa taifa hili. Alisema Ashton.

Kulegezwa kwa vikwazo dhidi ni ya Myanmar kunaonekana kama ni matokeo ya mvuto wa kisiasa yanayotokana na fursa ya kuingia bungeni kwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi ambaye chama chake kilishinda uchaguzi mdogo wa Ubunge Aprili mosi mwaka huu. Hata hivyo Suu Kyi amekataa kuingia bungeni hadi hapo hati ya kiapo cha ubunge itakapobadilishwa.

Wasiwasi juu ya Mtafaruku wa kisiasa

Kitendo cha Chama cha National League for Democracy NLD kukataa kiapo cha kulinda katiba ya nchi hiyo kimepingwa vikali na kimezusha mtafaruku ndani ya chama hicho, serikali na bunge la nchi hiyo ambapo wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wanasema kuwa kila upande hautaki suluhu na hakuna ajuaye namna hasa ya kuutatua.

Hali hiyo ambayo kiini chake ni msimamo wa NLD kutaka mabadiliko ya katiba yatakayopunguza uwezekano wa wanajeshi kuwa na usemi mkubwa katika siasa za nchi hiyo, haueleweki vizuri na mataifa ya magharibi yanayotaka kuimarika kwa hali ya kisiasa nchini humo.

Mazungumzo na Aung San Suu Kyi

Ashton anatarajiwa kulizungumzia suala hilo katika mazungumzo yake na Suu Kyi hii leo na kufungua ofisi ya Umoja wa Ulaya katika mji Mkuu wa nchi hiyo Yangoon ambayo itakuwa ni alama ya mwanzo ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya pande hizo mbili baada ya miaka 49 ya utawala wa kikatili wa kijeshi.

Aung San Suu Kyi wakati wa kampeni za uchaguzi wa bunge
Aung San Suu Kyi wakati wa kampeni za uchaguzi wa bungePicha: Reuters

Aidha, atakwenda pia katika mji mwingine wa Naypyitaw kukutana na Rais Thein Sein na washirika wengine wanaoonekana kuwa chachu ya mabadiliko ya kisiasa nchi humo akiwemo msemaji mdogo wa bunge la nchi hiyo Thra Shwe Mann na waziri wa Uchukuzi Aung Min ambaye amesaidia katika makubaliano mbalimbali ya kusitisha mapigano ya kikabila.

Ziara hii ya Ashton inakuja wakati huu ambapo Umoja wa Ulaya iko katika mchakato pamoja na mataifa ya magharibi yenye nguvu kiuchumi wa kupata hamasa na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na mataifa ya Kusini mwa Asia.

Mwandishi: Stumai George

Mhariri: Daniel Gakuba