1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa zamani wa polisi DRC atishia mapinduzi

12 Oktoba 2023

Maneno makali ya John Numbi dhidi ya rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi limejiri wakati wawaniaji urais wakiwasilisha fomu zao. Aliyoyasema Numbi yanaweza kuwakera washirika wa Tshisekedi.

https://p.dw.com/p/4XSol
Inspekta mkuu wa zamani wa polisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo John Numbi
Inspekta mkuu wa zamani wa polisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo John NumbiPicha: JUNIOR KANNAH/AFP/Getty Images

Inspekta mkuu wa zamani wa polisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo John Numbi, hivi majuzi alimshambulia Rais Felix Tshisekedi akikaribia kutoa wito wa kufanyika mapinduzi nchini humo kwa madai kadhaa, yakiwemo Tshisekedi kutomudu uongozi wa nchi hiyo.

Matamshi ya Numbi yanakuja wakati ambapo wagombea urais wamewasilisha nyaraka zao za kutaka kuwania nafasi ya uongozi wa nchi hiyo katika uchaguzi wa mwezi Desemba.

Huenda aliyoyasema Numbi yasifanyike ila matamshi hayo, bado yanawatia hofu wandani wa Tshisekedi. 

John Numbi alikuwa na umuhimu mkubwa katika utawala wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo Joseph Kabila, ila ushawishi wake ulipungua Kabila alipopeana madaraka kwa Felix Tshisekedi.

Wagombea 24 wa Urais Kongo warejesha fomu

Kinyang'anyiro cha urais DRC

Sasa wakati ambapo Tshisekedi anaumaliza muhula wake na mbio za kumrithi zinaanza, aliyekuwa mkuu wa polisi Numbi, anapaza sauti yake tena.

Wanasiasa kadhaa mashuhuri pamoja na Tshisekedi mwenyewe wamewasilisha maombi yao ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Desemba 20 nchini humo.
Wanasiasa kadhaa mashuhuri pamoja na Tshisekedi mwenyewe wamewasilisha maombi yao ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Desemba 20 nchini humo.Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Miongoni mwao ni daktari wa wanawake na mshindi wa Tuzo ya Nobel Denis Mukwege, gavana wa zamani wa mkoa wa kusini mashariki wa Katanga Moise Katumbi na Martin Fayulu aliyekuwa mshindani wa karibu wa Tshisekedi katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Wakati huo kulikuwa na uvumi wa mkutano wa siri kati ya Felix Tshisekedi na rais aliyekuwa mamlakani Joseph Kabila ambaye chama chake cha PPRDM  bado kilikuwa na wingi bungeni.

Inadaiwa kwamba mkutano huo ulipelekea makubaliano ya kugawana mamlaka na wizi wa kura ili kumpa Tshisekedi ushindi.

Tshisekedi aitaka MONUSCO kuondoka haraka Kongo

Na sasa katika hotuba yake aliyoitoa mtandaoni, Numbi amemtuhumu Tshisekedi kwa kwenda kinyume na makubaliano hayo akisema ni mfisadi, anachochea ukabila na anapanda mbegu za kuwatenganisha Wakongo.

Martin Fayulu, mwanasiasa wa upinzani nchini Congo anayetarajiwa kushindana na Tshisekedi kuwania urais Disemba 2023.
Martin Fayulu, mwanasiasa wa upinzani nchini Congo anayetarajiwa kushindana na Tshisekedi kuwania urais Disemba 2023.Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/picture alliance

Miaka ya hivi karibuni imeshuhudia mapinduzi kutoka katika nchi nyingi za Afrika Magharibi huku nchi za Jamhuri ya Afrika ya Kati na Gabon zikishuhudia tawala za kijeshi pia.

Hofu ya mapinduzi Afrika

Hofu ya mapinduzi imetanda katika eneo zima la Afrika ya Kati huku marais wakibadilisha uongozi wa majeshi yao.

Mukwege akosoa matayarisho uchaguzi DRC

Ila mtaalamu wa masuala ya usalama Jean-Jacques Wondo anasema nafasi ya kutokea mapinduzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni ndogo mno akidai jeshi la FARDC nchini humo limegawika.

"Ni vigumu leo kufikiria mapinduzi ya kumuondoa madarakani rais nchini Kongo. Hii ni kwasababu ya jinsi jeshi lilivyo, kwa kuwa ni kama jeshi la wanamgambo," amesema Wondo.

Miongo kadhaa ya mapigano na vita vya kikanda imepelekea makubaliano ya kugawa madaraka na makundi kadhaa ya wanamgambo kujumuishwa katika jeshi.

Kama sheria, mengi ya makundi hayo yalitumwa kufanya kazi mbali na kambi zao za awali ili kuzuia muingiliano wa kiutendaji.

Waandishi: Philipp Sandner na Wendy Bashy

Tafsiri: Jacob Safari